Ushiriki mdogo katika kura ya maoni ya katiba nchini Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64392-ushiriki_mdogo_katika_kura_ya_maoni_ya_katiba_nchini_algeria
Kura ya maoni kuhusu katiba ya Algeria ilifanyika Novemba Mosi ambapo ni Waalgeria wachache sana waliojitokeza katika zoezi hilo. Taarifa zinasema ni takribani asilimi 24 tu ya wananchi walioshiriki katika kura hiyo ya maoni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 02, 2020 23:12 UTC
  • Ushiriki mdogo katika kura ya maoni ya katiba nchini Algeria

Kura ya maoni kuhusu katiba ya Algeria ilifanyika Novemba Mosi ambapo ni Waalgeria wachache sana waliojitokeza katika zoezi hilo. Taarifa zinasema ni takribani asilimi 24 tu ya wananchi walioshiriki katika kura hiyo ya maoni.

Kura ya maoni ya Algeria ilifanyika Novemba Mosi, siku ambayo ilisadifiana na mwaka wa 66 tokea yalipojiri Mapinduzi ya Waalgeria ambayo yalikuwa mwanzo wa mapambano ya kupigania uhuru wa nchi hiyo.

Kura hiyo ya maoni ilikuwa na lengo la kubadilisha katiba ambayo ni kati ya masalia ya utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika.

Ikumbukwe kuwa Bouteflika aliondoka madarakni Aprili 2019 kufuatia maandamano makubwa ya wananchi waliokuwa wanataka mabadiliko. Nafasi yake ilichukuliwa na  Abdelmadjid Tebboune, mwenye umri wa miaka 75, ambaye amechukua hatua kadhaa za kuleta mabadiliko katika muundo wa kisiasa nchini humo. Ili kuwavutia wapinzani  Rais Tebboune, aliahidi kuwa hatua yake muhimu ya marekebisho itakuwa ni kufanya mabadiliko muhimu na ya kimsingi katika katiba ya Algeria.

Rais wa zamani wa Algeria Abdelaziz Bouteflika

Kati ya malengo ya kuandikwa katiba mpya ya Algeria ni kuzuia nchi hiyo kurejea katika zama za utawala wa kidikteta wa mtu mmoja. Kwa msingi huo katiba mpya inabana muhula wa urais kuwa ni mihula miwili tu. Aidha katiba mpya inalenga kumpunguzia rais mamlaka na kulipa bunge uwezo zaidi na pia kuvipa vyombo vya mahakama uhuru wa utendaji kazi. Hali kadhalika katiba mpya inalenga kuwapa wananchi uhuru zaidi wa maoni na kujieleza.

Pamoja na hayo, kumekuwepo na mjadala mkubwa kuhusu mabadiliko ya katiba ya Algeria. Vyama vingi vya kisiasa vimepinga kufanyika kura ya maoni wakati huu. Wapinzani wanaamini kuwa kura ya maoni iliyofanyika ilikuwa hatua ya kimaonyesho tu.

Katika upande wa pili, waungaji mkono wa mabadiliko ya katiba na kura ya maoni wanasema matukio ya kisiasa Algeria katika mwaka mmoja uliopita yamekuwa ni ya kurudhisha na kwamba nchi hiyo sasa imeingia katika duru mpya ya uhai wake wa kisiasa katika kile ambacho wanakitaja kuwa ni 'Jamhuri ya Tano."

Aidha waungaji mkono wa kura ya maoni wanaamini kuwa, katiba mpya itahitimisha mgogoro wa kisiasa uliopo nchini humo. Hii ni katika hali ambayo wapinzani wanasema katiba mpya iliyopigiwa kura haitaweza kuleta mabadiliko ya kimsingi bali kile kitakachofanyika ni kuzaliwa upya mfumo uliopita wa kisiasa. Rais Abdelmadjid Tebboune, amedai kuwa, katiba mpya itaweka msingi imara wa mabadiliko katika nchi hiyo.

Kura ya maoni imefanyika Algeria huku hitilafu za kisiasa zikishadidi na nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inaendelea kushuhudia mgogoro wa kisiasa na kiuchumi.

Mbali na mgogoro wa ndani wa kisiasa, Algeria inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupungua kwa bei ya mafuta ghafi ya petroli jambo ambalo limeathiri vibaya uchumi wa nchi hiyo. Aidha Algeria imeingia katika mashindano ya silaha na jirani yake, Morocco.

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria

Fauka ya hayo nchi hiyo ina mpaka wa kilomita elfu moja na nchi jirani ya Libya ambayo inakumbwa na mgogoro mkubwa wa kiusalama. 

Katika upande mwingine pia hivi sasa Rais Abdelmadjid Tebboune, amelazwa hospitalini nchini Ujerumani na hali yake inaripotiwa kuwa mbaya. Nukta hiyo pia imechangia ushiriki mdogo katika kura ya maoni.

Kutokuwepo  Tebboune nchini kumepelekea wapinzani watumie fursa hiyo kudai kuwa hakuna uwezekano wa kuidhinishwa katiba iliyopigiwa kura.

Abdulali Zaraqi, mchambuzi wa kisiaasa na mhadhiri wa chuo kikuu anasema kuwa, kuna uwezekano serikali ya Algeria ikashindwa kuidhinisha katiba mpya kwa sababu rais amelazwa hospitalini Ujerumani. Iwapo katiba itidhinishwa bila kutiwa saini na rais wa nchi, hilo litahesabiwa kuwa ni kuivunjia heshima katiba hiyo.

Matokeo rasmi ya kura ya maoni bado hayajatangwa lakini ushiriki mdogo sana wa Waalgeria ni ishara ya mgawanyiko mkubwa uliopo baina ya serikali na wananchi. Kilicho wazi ni kuwa, Waalgeria waliowengi wanataka mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa kisiasia na pia wanasisitiza kuwa viongozi wote wakongwe, akiwemo Rais Tebboune, waondoke madarakani. 

Kwa msingi huo inalekea kuwa, katika siku za usoni Algeria itashuhudia misukosuko zaidi ya kisiasa na kijamii hadi pale matakwa ya wananchi waliowengi yatakapotekelezwa.