UN: Zaidi ya watu 1,000 wameuawa nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64686-un_zaidi_ya_watu_1_000_wameuawa_nchini_sudan_kusini
Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya elfu moja wameuawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 17, 2020 23:00 UTC
  • UN: Zaidi ya watu 1,000 wameuawa nchini Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya elfu moja wameuawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Hayo yalisemwa jana Jumanne na  David Shearer, Mkuu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini (UNMISS) na kuongeza kuwa, watu wengine 400 wametekwa nyara katika mapigano hayo hususan katika jimbo la mashariki la Jonglei.

Amesema mapigano hayo ya kikabila yanayaweka katika hatari ya kusambaratika makubaliano ya amani yaliyosainiwa Septemba mwaka 2018 baina ya Rais Salva Kiir na Riek Machar.

Mapigano hayo ya umwagaji damu yanaripotiwa katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Oktoba, serikali ya Sudan Kusini na makundi ya upinzani ziliahidi kwa mara nyingine kuheshimu Makubaliano ya Kusitisha Uhasama (COHA) katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika huko Rome.

Magenge ya waasi yanayumbisha usalama na amani ya Sudan Kusini

Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua. 

Vita vya ndani nchini humo vimeshasababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.