Waziri Mkuu wa Eswatini (Swaziland) aaga dunia kwa COVID-19
Ambrose Dlamini, Waziri Mkuu wa Eswatini (Swazilanda) ambaye alikuwa amelazwa hospitalini huko Afrika Kusini, ameaga dunia kutokana na virusi vya maradhi ya corona au COVID-19
Serikali ya Eswatini (Swaziland ya zamani) imetoa taarifa ikithibitisha kuaga dunia waziri mkuu huyo. Ambrose Dlamini aliyekuwa na umri wa miaka 52 alikuwa amelazwa hospitalini tokea mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba baada ya kuthibitika kuwa alikuwa ameambukizwa virusi vya corona.
Themba Masuku, Naibu Waziri Mkuu wa Eswatini, bila ya kutoa maelezo zaidi, amesema kwamba Dlamini aliaga dunia jana alasiri katika dospitali moja huko Afrika Kusini.
Dlamini ambaye alikuwa mfanyabiashara mashuhuri alichukua hatamu za uwaziri mkuu wa Eswatini mnamo Oktoba 2018.
Tokea virusi vya corona vienee duniani, kati ya watu milioni moja na elfu 140 wa Eswatini, watu 6,768 wameambukizwa na wengine 127 kupoteza maisha nchini humo kutokana na maradhi hayo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la nchi hiyo lililo na makao makuu yake huko Afrika Kusini kwa jila la Swaziland Solidarity Network SSN, lilikuwa limeikashifu serikali kwa kumpa waziri mkuu huyo huduma za upendeleo kwa kumpa matibabu katika nchi iliyo na huduma bora zaidi za matibabu na kutowajali raia wengine wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za miaka 2016 na 2017, asilimia 39 ya raia wa Eswatini walikuwa wanaishi chini ya mstari wa umasikini.