Makumi ya watoto wengine waliotekwa nyara Nigeria waokolewa
Jeshi la Polisi la Nigeria limetangaza habari ya kuwanusuru makumi ya wanafunzi waliotekwa nyara na watu waliobeba silaha siku ya Jumamosi.
Taarifa ya polisi ya Nigeria imesema kuwa, wanafunzi 84 walionusuriwa ni miongoni mwa makumi ya wengine waliotekwa nyara na watu wasiojulikana walipokuwa njiani kurejea nyumbani katika kijiji cha Mahuta wakitoka katika sherehe za kidini katika jimbo la Katsina, kaskazini magharibi mwa nchi.
Wanafunzi hao walinusuriwa kufuatia makabiliano makali ya risasi baina ya watekaji kwa upande mmoja, na maafisa usalama na makundi yanayobeba silaha katika kijiji hicho kwa upande mwingine. Hili ni tukio la pili la kutekwa nyara wanafunzi katika jimbo la Katsina ndani ya siku nane.
Polisi katika jimbo la Katsina imeripoti kuwa, watoto 80 miongoni mwa makumi waliotekwa ni wanafunzi wa Shule ya Kiislamu ya Hizburrahim Islamiyya.
Ijumaa iliyopita, vyombo vya usalama vya Nigeria vilitangaza habari ya kuachiwa huru karibu wanafunzi wavulana 350 kati ya 520 wa shule ya upili ya eneo la Kankara kaskazini magharibi mwa nchi, waliokuwa wametekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram.
Haikubainika wanafunzi hao waliachiwa huru katika mazingira gani, lakini serikali ilisisitiza kuwa haikutoa kikomboleo cha kuachiwa huru watoto hao kwa genge hili la ukufurishaji. Kabla ya tukio hili la Kankara, mwaka 2014 kundi hilo la kigaidi liliwateka nyara pia wanafunzi wa kike 200 huko Nigeria.