Wabunge wa Algeria wataka iwe jinai kuanzisha uhusiano na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65660-wabunge_wa_algeria_wataka_iwe_jinai_kuanzisha_uhusiano_na_israel
Makumi ya wabunge wa Algeria wameandaa muswada wa sheria inayopania kuufanya kuwa ni uhalifu uanzishwaji wa uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2021 23:11 UTC
  • Wabunge wa Algeria wataka iwe jinai kuanzisha uhusiano na Israel

Makumi ya wabunge wa Algeria wameandaa muswada wa sheria inayopania kuufanya kuwa ni uhalifu uanzishwaji wa uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Yousuf Adjissa, mwanachama wa Harakati ya Jamuiya ya Amani, ambacho ni chama kikubwa zaidi cha Kiislamu nchini Algeria, ameukabidhi muswada huo kwa Rais wa Bunge la nchi hiyo, kwa niaba ya wabunge zaidi ya 50 wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina la Shehab, muswada huo una vipengee saba, na cha kwanza kinasema: Lengo ni kukufanya kuwa ni kosa la uhalifu kuanzisha uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Kipengee hicho kimeeleza kuwa, ni marufuku kuwasiliana, kuanzisha uhusiano wa aina yoyote, au kufungua ofisi za kibalozi za kiwango chochote ile katika utawala wa Kizayuni, kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

Kipengee kingine cha muswada huo kinasema, hairuhusiwi kusafiri kwenda au kutoka katika utawala wa Kizayuni, na pia ni marufuku kuingia au kupewa uraia na utawala huo katika ofisi yoyote ile ya kibalozi ya Algeria.

Bunge la Algeria

Yousuf Adjissa amesisitiza kuwa, lengo la kutunga sheria hiyo ni kuhakikisha pia kwamba kufanya biashara au miamala yoyote ya kiuchumi na utawala wa Kizayuni pamoja na mashirika ya utawala huo haramu kunahesabiwa kuwa ni kosa la uhalifu.

Katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka uliomalizika wa 2020, nchi nne za Kiarabu za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zilianzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Kizayuni na Israel. Hatua hiyo ya kihaini na ya usaliti iliyofanywa na nchi hizo ambayo ni kushiriki kwenye mpango wa mapatano wa Kimarekani na Kizayuni, imelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.