Uganda kuondoa askari wake wa kulinda amani Somalia?
Huenda Uganda ikaondoa wanajeshi wake wanaolinda amani nchini Somalia chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.
Luteni Kanali Paddy Ankunda, msemaji wa jeshi la Uganda amesema tayari kamati maalumu imebuniwa kutathmini iwapo askari hao wa Uganda wataondolewe nchini Somalia au na kwamba mapendekezo ya kamati hiyo yatatekelezwa na serikali. Duru za habari zimedokeza kuwa, yumkini uamuzi huo ukaathiri wanajeshi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki wanaolinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hata hivyo haijabainika sababu za serikali ya Kampala kutathmini kuondoa askari wake zaidi ya elfu sita nchini Somalia.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, hivi karibuni Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa utapunguza asilimia 20 ya misaada yake ya kifedha kwa kikosi cha AMISOM.
Askari elfu 22 wa Afrika walitumwa nchini Somalia miaka 9 iliyopita kwa ajili ya kurejesha amani na kukabiliana na kundi la kigaidi la al-Shabaab. Mbali na Uganda, nchi zingine ambazo zimetuma askari nchini Somalia chini ya AMISOM ni Burundi, Ethiopia, Kenya na Djibouti.
Mfuko wa kusaidia amani barani Afrika unaosimamiwa wa Umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka 9 iliyopita umechangia uro zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya AMISOM.