Afrika yaagiza dozi milioni 400 zaidi za Covid-19
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66226-afrika_yaagiza_dozi_milioni_400_zaidi_za_covid_19
Kituo cha Umoja wa Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (Africa-CDC) kimesema bara hilo limefanikiwa kuagiza dozi milioni 400 za chanjo za Covid-19 zaidi, baada ya kuagiza dozi milioni 270 za chanjo hizo hapo awali.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jan 29, 2021 04:08 UTC
  • Afrika yaagiza dozi milioni 400 zaidi za Covid-19

Kituo cha Umoja wa Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (Africa-CDC) kimesema bara hilo limefanikiwa kuagiza dozi milioni 400 za chanjo za Covid-19 zaidi, baada ya kuagiza dozi milioni 270 za chanjo hizo hapo awali.

Dozi hizo mpya milioni 400 ni za shirika la Oxford-AstraZeneca la Uingereza na Taasisi ya Serum ya India. Hata hivyo taarifa ya Africa-CDC haijaeleza juu ya thamani na gharama ya chanjo hizo.

John Nkengasong, Mkuu wa Afrika-CDC amesema kampeni za kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 katika nchi za bara la Afrika zinatamiwa kuanza mwezi Machi mwaka huu, na kwamba kiwango kikubwa cha dozi hizo za corona kinatazamiwa kuwasili barani humo mwishoni mwa mwaka huu 2021.

Afrika inahitaji dozi bilioni 1 na laki 5 ili iweze kuchanja asilimia 60 ya wakazi wa bara hilo. Hapo awali Africa-CDC ilisema jumla ya dozi bilioni 1.5 za chanjo ya Covid-19 zinahitajika barani Afrika na inakadiriwa kuwa zitagharimu dola bilioni 10.

Takwimu za Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) zinaonyesha kuwa, hadi sasa kuna kesi karibu milioni 4 zilizothibitishwa kuwa na maambukuzi ya virusi vya corona au Covid-19 barani Afrika. Aidha takwimu za Africa CDC zinaonyesha kuwa, hadi sasa watu karibu 90 elfu wamepoteza maisha kutokana na corona barani humo, huku idadi ya watu waliopata afueni baada ya kuambukizwa ugonjwa huo barani humo hadi sasa kufikia karibu milioni 3.

Chanjo ya corona

Katika hatua nyingine, Mawaziri wa Afya na Fedha wa ara la Afrika wanatazamiwa kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya duniani (WHO), Dkt Tedros Ghebreyesus, kujadili suala la ugawaji sawa wa chanjo za Covid-19. Ameeleza bayana kuwa, ”nitawaambia kuwa tunafanya kila tuwezalo kufanikisha kuanza kwa utoaji chanjo barani Afrika, kuokoa maisha na kurejesha uchumi, kinachobakia ni dunia inapaswa itekeleza jukumu lake."

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), kuyasihi mataifa tajiri kutoa dozi za ziada za chanjo za corona kwa nchi zilizo masikini na zinazoendelea.