Usalama umerejea katika mji wa Bangassou Jamhuri ya Afrika ya Kati
Shughuli za kibiashara zimerejea tena katika mji wa Bangassou, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR baada ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wa ujumbe wa umoja huo nchini humo, MINUSCA kuimarisha doria ili kudhibiti vitisho vyovyote kutoka kwa waasi waliosababisha maelfu ya watu kukimbia makwao kufuatia mashambulizi ya mwezi uliopita wa Januari.
Itakumbukwa kuwa mji wa Bangassou, ulioko kandokando ya mto Mbomou, kilometa 750 kutoka mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, ulikuwa kitovu cha mashambulizi yaliyofanywa na kikundi cha waasi wa CPC tarehe 3 mwezi uliopita wa Januari.
Wiki mbili baada ya shambulio hilo, hali ya hatari ilitangazwa na kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSCA na waasi hao walikimbia mji huo.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, kwa sasa MINUSCA na askari wa jeshi la serikali wanaudhibiti mji wa Bangassou na kutoa hakikisho la usalama wa raia pamoja na taasisi za umma kutokana na doria zao.
Kanali Nourdinne Amaraoui ambaye ni kamanda na kikosi cha Morocco kinachohudumu ndani ya MINUSCA mjini Bangassou amesema, amani na utulivu vimerejea mjini humo na pia shughuli za biashara zinaendelea, lakini akatahadharisha kwamba, hiyo haimaanishi kuwa waasi wametoweka kikamilifu.

Jessy Ndassi, ambaye ni mkazi wa eneo la Tokoyo amesema, wakati yalipofanyika mashambulizi ya waasi, wananchi walikimbia mji, lakini sasa amani imeanza kurejea na shughuli zinarejea na soko la eneo hilo limefunguliwa.
Ripoti zinaeleza kuwa, hivi sasa usalama umeimarishwa zaidi kwa kuweka vituo vipya ikiwemo katika mto Mbomou ambao ndio mpaka wa pamoja wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Aidha kikosi cha askari wa Rwanda wanaohudumu katika MINUSCA kimeongeza zaidi ufuatiliaji wa usalama wa raia kwa kutumia ndege zisizo na rubani au drone.../