Maajenti 12 wa usalama wauawa katika shambulio la bomu Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66616-maajenti_12_wa_usalama_wauawa_katika_shambulio_la_bomu_somalia
Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Somalia pamoja na maajenti 11 wa kitengo hicho cha usalama wameuawa katika mripuko wa bomu la kutegwa kando ya barabara katika jimbo la Galmudug, katikati ya nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2021 08:41 UTC
  • Maajenti 12 wa usalama wauawa katika shambulio la bomu Somalia

Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Somalia pamoja na maajenti 11 wa kitengo hicho cha usalama wameuawa katika mripuko wa bomu la kutegwa kando ya barabara katika jimbo la Galmudug, katikati ya nchi.

Mohamed Ahmed, afisa wa polisi katika eneo hilo amesema Abdirashid Abdunur Qoje, Mkuu wa Idara ya Intelijensia wa nchi hiyo ameuawa pamoja na walinzi wake katika shambulio hilo la kigaidi.

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, mripuko huo ulitokea jana Jumapili katika eneo la Eldhere, umbali wa kilomita 30 kaskazini mwa mji wa Dhusamareb, jimboni Galmudug. Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limetangaza kuhusika na hujuma hiyo. 

Wanasiasa wa Somalia wamekuwa wakikutana mjini hapo kwa siku kadhaa sasa, kujaribu kutanzua kitendawili cha uchaguzi wa rais unaopaswa kufanyika leo.

Rais wa Somalia anayeondoka, Muhammed Abdullahi Farmajo 

Baraza la wagombea urais wa vyama vya upinzani nchini humo limetangaza katika taarifa kuwa, kuanzia leo Februari 8, halitamtambua Muhammed Abdullahi Farmajo kuwa Rais halali wa Somalia. Farmajo ambaye muhula wake wa kuhudumu kama rais wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika unamalizika rasmi leo amelitaka Bunge la nchi hiyo liingilie kati ili nchi hiyo isitumbukie katika mgogoro wa kikatiba. 

Anasema uingiliaji wa madola ajinabi katika mambo ya ndani ya nchi hiyo ndiyo sababu kuu ya kugonga mwamba mazungumzo ya kujaribu kuupatia ufumbuzi mkwamo wa uchaguzi katika nchi hiyo.