Rwanda: Kuifunga Kigali kumezuia maambukizi ya corona kwa 72%
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66678-rwanda_kuifunga_kigali_kumezuia_maambukizi_ya_corona_kwa_72
Serikali ya Rwanda imesema hatua yake ya kuweka zuio la kutoka nje katika mji mkuu Kigali kwa lengo la kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona imezaa matunda, na kwamba maambukizi ya virusi hivyo katika mji mkuu huo yamepungua kwa asilimia 72.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2021 23:00 UTC
  • Rwanda: Kuifunga Kigali kumezuia maambukizi ya corona kwa 72%

Serikali ya Rwanda imesema hatua yake ya kuweka zuio la kutoka nje katika mji mkuu Kigali kwa lengo la kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona imezaa matunda, na kwamba maambukizi ya virusi hivyo katika mji mkuu huo yamepungua kwa asilimia 72.

Hayo yamesemwa na Dakta Sabin Nsanzimana, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Tiba cha Rwanda (RBC) katika ujumbe wake aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: Natija ya kulifunga jiji la Kigali kwa siku 21 ni ya kuridhisha.

Serikali ya Rwanda iliondoa agizo hilo juzi Jumatatu Februari 8 na kuwaruhusu wakazi wa Kigali kurejea katika shughuli zao za kawaida, lakini baadhi ya hatua kama agizo la kutotoka nje nyakati za usiku, marufuku ya mikusanyiko, kunawa mikono na kuvaa barakoa zingali zinazingatiwa.

Serikali ya Rwanda ikitoa misaada kwa walioathiriwa na zuio la kutoka nje Kigali

Januari 18, Rwanda ilitangaza kufunga shule zote zikiwemo za chekechea katika mji mkuu Kigali kutokana na ongezeko la kesi za maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 mjini hapo.

Rwanda ilichukua hatua hiyo pamoja na ya kulifunga jiji hilo kwa wiki tatu, baada ya takwimu za Wizara ya Afya ya nchi hiyo kuonesha kuwa, asilimia 60 ya kesi za corona zilizonakiliwa nchini humo kati ya Januari Mosi na Januari 15, ziliripotiwa Kigali.