Mabaharia wa Uturuki waliotekwa nyara Nigeria warejea nyumbani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66850-mabaharia_wa_uturuki_waliotekwa_nyara_nigeria_warejea_nyumbani
Mabaharia 15 wa Uturuki waliotekwa nyara mwezi uliopita katika Ghuba ya Guinea wamerejea nyumbani leo Jumapili huku nahodha wao akisema walikabiliwa na vitisho vya kuuawa wakati waliposhikiliwa kwa muda wa wiki tatu msituni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2021 09:27 UTC
  • Mabaharia wa Uturuki waliotekwa nyara Nigeria warejea nyumbani

Mabaharia 15 wa Uturuki waliotekwa nyara mwezi uliopita katika Ghuba ya Guinea wamerejea nyumbani leo Jumapili huku nahodha wao akisema walikabiliwa na vitisho vya kuuawa wakati waliposhikiliwa kwa muda wa wiki tatu msituni.

Mabaharia hao waliwasili leo asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul na kulakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, familia zao na maafisa wengine, siku mbili baada ya kuachiliwa huru nchini Nigeria.

Maharamia waliwateka mabaharia hao mnamo Januari 23  karibu na kisiwa cha Sao Tome wakati meli yao yenye bendera ya Liberia ilipokuwa ikielekea Cape Town kutoka Lagos.

Maharamia waliiachia huru meli lakini wakawachukua mateka mabaharia15 wa Uturuki na kumuua baharia kutoka Jamhuri ya Azerbaijan.

Kwa mujibu wa Idara ya Shirika la Kimataifa la Usafiri Baharini, Ghuba ya Guinea, ambayo iko katika pwani za Nigeria, Guinea, Togo, Benin na Cameroni, kwa sasa ni eneo hatari zaidi baharini kutokana na ongezeko kubwa la uharamia.

Julai 2019, mabahari 10 wa Uturuki walitekwa nyara katika pwani ya Nigeria na kuachiliwa huru baada ya mwezi moja.