Mripuko mpya wa tauni waua watu 31 Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67074
Mripuko mpya wa ugonjwa angamizi wa tauni umeibuka kaskazini mashariki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo hadi sasa watu zaidi ya 30 wanaripotiwa kupoteza maisha.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 20, 2021 13:26 UTC
  • Mripuko mpya wa tauni waua watu 31 Kongo DR

Mripuko mpya wa ugonjwa angamizi wa tauni umeibuka kaskazini mashariki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo hadi sasa watu zaidi ya 30 wanaripotiwa kupoteza maisha.

Patrick Karamura, Waziri wa Afya katika mkoa wa Ituri alisema hayo jana Ijumaa na kueleza kuwa, hadi sasa kesi zaidi ya 500 za maradhi hayo zimenakiliwa, mbali na vifo 31 tokea mripuko huo mpya uripotiwa kaskazini mashariki mwa DRC yapata miezi mitatu iliyopita.

Wataalamu wa afya nchini humo wamesema aghalabu ya kesi hizo zilirekodiwa baina ya Novemba 15 na Disemba 13 mwaka jana, na kwamba wastani wa umri wa waathirika ni miaka 13.

Shirika la Afya Duniani (WHO) mwezi Julai mwaka jana lilitoa indhari ya kuibuka mripuko wa tauni katika mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mkoa huo umekuwa ukishuhudia miripuko ya mara kwa mara ya tauni, tangu mripuko wa kwanza uripotiwe katika mkoa huo mwaka 1926.

Kisiwa cha Madagascar cha kusini mashariki mwa Afrika kishawahi kumbwa pia tauni miaka kadhaa nyuma

Machi mwaka 2019, mripuko mwingine wa tauni uliibuka katika mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo watu kadhaa walipoteza maisha. 

Hayo yanajiri wakati ambao wakuu wa DRC wangali wanakabiliana na mripuko mpya wa ugonjwa hatari wa Ebola na maradhi angamizi ya kuambukiza ya Covid-19.