Oct 04, 2024 07:13 UTC
  • Makumi waaga dunia katika ajali ya boti mashariki ya DRC

Zaidi ya watu 70 wamekufa maji baada ya boti waliokuwa wakisafiria kupinduka kwenye Ziwa Kivu jana Alkhamisi, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, karibu na Rwanda.

Jean-Jacques Purisi, Gavana wa Kivu Kusini amesema boti hiyo ilikuwa ikielekea Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini, ikitokea Minova katika jimbo la Kivu Kusini wakati ilipozama katika kijiji cha Mukwidja katika eneo la Kalehe kwenye maji ya Ziwa Kivu.

"Boti hiyo ilikuwa imebeba zaidi ya watu 200, ingawa ina uwezo wa kubeba takriban abiria 30 pekee," Purusi aliwaambia waandishi wa habari na kuongeza kuwa, "Miili 78 imeopolewa majini kufikia sasa. Hatuna idadi ya kamili ya walioaga dunia kwa kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba watu 278."

Mashuhuda wa ajali hiyo wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema, zaidi ya miili 30 imeopolewa majini, na kwamba takriban watu 60 wamenusurika.

Mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, watu zaidi ya 100 walikufa maji baada ya boti iliyokuwa imewabeba kupinduka na kuzama magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ajali hiyo imetokea miezi miwili baada ya boti nyingine kuzama na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 80 katika mto Kwa, magharibi ya Kongo DR.

Ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika maji ya Kongo hususan kutokana na kuwa vyombo vingi vya majini hupakia watu kupita kiasi. Nchi hiyo ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na usafiri mkubwa ni wa majini.

Tags