Waliokufa maji katika ajali za boti 2 DRC wapindukia 50
Watu wasiopungua 52 wamethibitishwa kufariki dunia huku wengine kadhaa wakitoweka baada ya boti mbili za abiria kuzama kwenye maji ya Ziwa Tumba, magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Maafisa wa serikali walisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, boti hizo zilizama usiku wa kuamkia Alkhamisi karibu na Bikoro, takriban kilomita 128 (maili 79) kutoka Mbandaka katika jimbo la Equateur.
Dieu Merci Akula Mboyo, Afisa wa Uratibu wa Jopo la Wataalamu wa Asasi za Kiraia katika Mkoa wa Equateur amesema idadi ya muda iliyothibitishwa ya vifo ni 52.
"Ajali hizo zilisababishwa na kujaa abiria kupindukia, na upepo mkali huku kukiwa na mvua kubwa," Mboyo aliwaambia waandishi wa habari huko Bikoro jana Ijumaa. Ameongeza kuwa, waendeshaji wa boti hizo hapo awali walikataa kubeba abiria zaidi, lakini mwishoye walikubali shinikizo.
Mboyo ametaka kufanyika uchunguzi wa serikali kama moja wapo ya njia za uwajibikaji na kuzuia majanga katika siku zijazo.
Mapema siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Mkoa wa Equateur, Chrispin Moliy alisema serikali za majimbo na kitaifa zitahakikisha miili iliyopatikana inafanyiwa mazishi yanayofaa.
Idadi kamili ya watu waliotoweka kwenye ajali hizo bado haijathibitishwa na mamlaka, lakini vyombo vya habari vya ndani vilikadiria takriban watu 100 walikuwa kwenye vyombo hivyo vya usajfiri wa majini.