Sep 30, 2024 02:25 UTC
  • WHO kuisaidia Rwanda kukabiliana na mripuko wa kwanza wa Marburg

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaka jamii ya kimataifa ishirikiane na Rwanda katika kupambana na mripuko wa kwanza wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Marburg (MVD).

WHO imesema inaandaa timu ya wataalamu watakaotumwa Rwanda wakiwa wamejizatiti kwa vifaa tiba kwenda kuisaidia nchi hiyo kudhibiti usambaaji wa ugonjwa huo.

Idara ya Dharura ya WHO huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya imesema, vifaa vya kuzuia kuenea kwa maradhi hayo vitawasili Kigali, mji mkuu wa Rwanda ndani ya siku chache zijazo.

Dakta Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO barani Afrika amesema, "Tunaandaa suhula zote zinazohitajika kwa ajili ya kudhibiti mripuko wa Marburg nchini Rwanda kwa njia ya haraka."

Rwanda imethibitisha vifo sita na kesi 20 za ugonjwa wa Marburg tangu kuripotiwa mripuko huo.

Waziri wa Afya wa Rwanda, Sabin Nsanzimana amesema aghalabu ya waathiriwa wa virusi hivyo ni wafanyakazi wa afya hasa wanaohudumu katika sadaruki (chumba cha wagonjwa mahututi). 

Ugonjwa wa Marburg husababishwa na virusi vinavyoshabihiana na Ebola na hata dalili zake hazina tofauti kubwa na ugonjwa wa Ebola. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuharisha na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu mwilini.

Tags