Nigeria: Watekajinyara wamewaachia huru watu 53 katika jimbo la Niger
Kundi la wahalifu lililokuwa limewashikia mateka watu 53 limewaachia huru mateka hao wakiwemo wanawake na watoto waliotekwa kwenye basi nchini Nigeria.
Maafisa wa serikali ya Nigeria wameeleza kuwa, makumi mengine ya watu waliotekwa nyara shuleni katika tukio kama hilo bado hawajulikani walipo.
Magenge ya uhalifu anayotajwa kuwa ni majambazi huko Kaskazini Magharibi na katikati mwa Nigeria yamezidisha mashambulizi na hujuma katika miaka ya karibuni ikiwemo kuteka nyara watu, kubaka na kupora mali za raia.
Wiki iliyopita genge moja la wahalifu liliwateka nyara raia 53 wakiwemo wanawake na watoto waliokuwa wakisafiri kuelekea kijiji cha Kindu, jimboni Niger kwa kutumia usafiri wa basi inayomilikiwa na serikali.
"Nimefurahi kusikia taarifa ya kuachiwa huru raia 53 waliokuwa wakisafiri kwa basi na kisha kutekwa nyara na majambazi wiki mja iliyopita", amesema Abubakari Sani Bello Gavana wa Jimbo la Niger.
Msemaji wa Gavana wa Jimbo la Niger, Mary Noel Berje amesema kuwa, hadi sasa bado haijafahamika kama mlungura ulitolewa kwa ajili ya kukombolewa mateka hao lakini wawakilishi wa jimbo hilo hivi karibuni waliweka wazi kwamba hawatataoa chochote kwa watekaji nyara.
Bi Mary ameongeza kuwa, walifanya mazungumzo kwa muda wa wiki moja ikiwa ni pamoja na mashauriano bila kulala kwa sababu walipasa kuhakikisha kuwa, raia hao wanaachiwa huru haraka iwezekanavyo.
Abiria hao walioachiwa huru wanaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari ili kujua hali zao za kiafya kabla ya kuunganishwa na familia zao.
Katika tukio jingine wiki iliyopita, watu 42 wakiwemo wanafunzi wa kiume 27 walitekwa nyara shuleni huko Nigeria na hadi sasa hawajulikani walipo.