Mamia ya wanafunzi wa kike watekwa nyara katika jimbo la Zamfara, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67292-mamia_ya_wanafunzi_wa_kike_watekwa_nyara_katika_jimbo_la_zamfara_nigeria
Majambazi waliokuwa na silaha leo asubuhi wameivamia shule moja ya sekondari ya wasichana katka jimbo la Zamfara nchini Nigeria na kuwateka nyara mamia ya wanafunzi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 26, 2021 09:32 UTC
  • Mamia ya wanafunzi wa kike watekwa nyara katika jimbo la Zamfara, Nigeria

Majambazi waliokuwa na silaha leo asubuhi wameivamia shule moja ya sekondari ya wasichana katka jimbo la Zamfara nchini Nigeria na kuwateka nyara mamia ya wanafunzi.

Shambulio hilo limefanywa katika shule ya sekondari ya wasichana ya Jangebe inayomilikiwa na serikali katika eneo la Talata Mafara jimboni Zamfara. Mwalimu mmoja wa shue hiyo amethibitisha kujiri shambulio hilo na kueleza kuwa, wanafunzi wasichana karibu 300 wametekwa nyara na genge la watu waliokuwa na silaha mapema leo asubuhi.  

Jimbo la Zamfara  

Zamfara, jimbo linalopatikana Kaskazini Magharibi mwa Nigeria, ni moja kati ya majimbo ya nchi hiyo yaliyoathiriwa pakubwa na mashambulzi na hujuma mbalimbali za magenge ya uhalifu yanayobeba silaha. Mashambulizi hayo yamekuwa yakiendelea licha ya mazungumzo yaliyoanzishwa na serikali kuu ili kufikia mapatano na magenge hayo. 

Shambulio la karibuni zaidi lilijiri wiki mbili baada ya wanafunzi 20 kutekwa nyara na wanamgambo wenye silaha huko katika jimbo la Niger.  

Genge la watu waliokuwa na silaha Jumatatu wiki hii liliwaachia huru mateka 53  wakiwemo wanawake na watoto liliowateka nyara kwenye basi nchini Nigeria wiki iliyopita. 

Mbali na kushambuliwa shule hiyo ya sekondari ya wasichana na kutekwa nyara mamia ya wanafunzi, hivi karibuni pia kundi la kigaidi la Boko Haram liliwateka nyara wanafunzi wavulana 520 katika shule ya upili ya eneo la Kankara Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.