Mamia ya wanafunzi waliotekwa nyara Nigeria waachiliwa huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67428-mamia_ya_wanafunzi_waliotekwa_nyara_nigeria_waachiliwa_huru
Mamia ya wanafunzi wa kike waliotekwa nyara huko Nigeria katika jimbo la Zamfara wameachiliwa huru.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 02, 2021 04:16 UTC
  • Mamia ya wanafunzi waliotekwa nyara Nigeria waachiliwa huru

Mamia ya wanafunzi wa kike waliotekwa nyara huko Nigeria katika jimbo la Zamfara wameachiliwa huru.

Ghavana Bello Matawalle wa jimbo la Zamfara Nigeria ametuma ujumbe wa Twitter mapema leo Jumanne na kusema wasichana hao wa shule ya upili katika eneo la Jangebe wameachiliwa huru na wanamgambo waliokuwa wamewateka nyara.

Wasichana hao walitekwa nyara Ijumaa na wanamgambo walioishambulia shule hiyo ya bweni katika tukio la pili la utekaji nyara kaskazini mwa Nigeria katika kipindi cha wiki moja.

Zamfara, jimbo linalopatikana Kaskazini Magharibi mwa Nigeria, ni moja kati ya majimbo ya nchi hiyo yaliyoathiriwa pakubwa na mashambulzi na hujuma mbalimbali za magenge ya uhalifu yanayobeba silaha. Mashambulizi hayo yamekuwa yakiendelea licha ya mazungumzo yaliyoanzishwa na serikali kuu ili kufikia mapatano na magenge hayo. 

Mbali na kushambuliwa shule hiyo ya sekondari ya wasichana na kutekwa nyara mamia ya wanafunzi, hivi karibuni pia kundi la kigaidi la Boko Haram liliwateka nyara wanafunzi wavulana 520 katika shule ya upili ya eneo la Kankara Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.