Wapinzani Kenya wakaidi amri na kuandamana kupinga tume ya uchaguzi
(last modified Mon, 09 May 2016 15:19:59 GMT )
May 09, 2016 15:19 UTC
  • Wapinzani Kenya wakaidi amri na kuandamana kupinga tume ya uchaguzi

Wafuasi wa muungano wa upinzani wa Cord nchini Kenya wamekaidi amri ya serikali na kuibua ghasia nje ya makao makuu ya Tume Huru ya Uchaguzi IEBC mjini Nairobi.

Viongozi wa Cord Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetang’ula wamewakusanya wafuasi wao kuandamana na kuibua machafuko mjini Nairobi huku polisi wa kuzima ghasia wakilinda ofisi za IEBC zilizo karibu na Chuo Kikuu cha Nairobi.

Vinara wa Cord Odinga na Musyoka wamedai kuwa tume hiyo inapanga kuiba uchaguzi mkuu mwakani kwa maslahi ya muungano tawala wa Jubilee na hivyo wameitaka ijiuzulu.

Ripoti zinasema baadhi ya waliokuwa wakishiriki katika maandamano hayo wametumia fursa hiyo kuwaibia wapita njia na kupora baadhi ya maduka. Wafanya biashara wengi wamelazimika kufunga biashara zao katika eneo la kati kati mwa jiji la Nairobi kwa kuhofia kuibiwa mali zao.

Maandamano pia yameripotiwa katika mji wa Kisumu ambao ni ngome ya Raila Odinga na pia katika ofisi za IEBC maeneo kadhaa nchini Kenya.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya Ishaq Hassan amekanusha vikali madai ya Cord kuwa tume hiyo inapanga kuiba uchaguzi na amewataka wanaotoa madai kama hayo kuleta ushahidi.

Tags