Tanzania kuisaidia Burundi kujiunga na jumuiya ya SADC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi ameiahidi nchi ya Burundi kuwa Tanzania itashirikiana nayo katika harakati zake za kuomba kujiunga na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kabudi ametoa ahadi hiyo leo mkoani Kigoma kwenye mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi.
Amesema Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidugu baina ya nchi hizo mbili kama njia mojawapo ya kuwaenzi waasisi wake.
Ameeleza bayana kuwa, “njia pekee ya kuwaenzi waasisi wa mataifa haya mawili ni kuimarisha uhusiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi, kijamii na masuala ya usalama.”
Agosti mwaka jana, Tanzania iliikabidhi Msumbiji uwenyekiti wa SADC wakati jumuiya hiyo ya kikanda ilikuwa ikiadhimisha miaka 40 tangu kuasisiwa kwake.
Itakumbukwa kuwa, miaka kadhaa iliyopita, Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC iliitaka Burundi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliokuwa ukiikabili, iwapo inataka kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.