Watu 13 wauawa katika shambulio la wabeba silaha nchini Nigeria
Watu wasiopungua 13 wamepoteza maisha katika mashambulizi ya genge la wabeba silaha katika jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria.
Samuel Aruwan, Kamishna wa Usalama wa Ndani na Mambo ya Ndani ya Kaduna ameripoti kwamba watu wasiojulikana wamefanya mashambulizi ya kuvizia katika wilaya za Zangon Kataf, Chikun na Karu mkoani hapo na kuuawa watu 13. Aruwan amebainisha kuwa, mbali na watu 13 kuuawa katika hujuma hiyo, wengine zaidi ya 7 wamejeruhiwa.
Amesema kuwa nyumba 56 na pikipiki 16 ziliteketezwa moto katika mashambulizi hayo, na kwamba wakazi wa mkoa huo wamekimbia makazi yao wakihofia kushambuliwa.
Hii ni katika hali ambayo, makumi ya watu waliuawa katika shambulizi lililotekelezwa na watu wenye silaha siku mbili zilizopita katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.
Wiki iliyopita, kundi la kigaidi la ISIS tawi la Afrika Magharibi lilitangaza kuhusika na shambulio dhidi ya msafara wa magari ya kijeshi lililoua na kujeruhi watu zaidi ya 30 huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria anaendelea kukosolewa kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kuyatokomeza makundi ya kigaidi na ya wabeba silaha nchini humo ambayo mbali na kuua na kujeruhi maafisa usalama na raia wasio na hatia, lakini pia yanateka nyara wanafunzi kila uchao.