Mahakama ya Katiba ya Niger 'yabariki' ushindi wa Mohamed Bazoum
Mahakama ya Katiba ya Niger imeidhinisha ushindi wa matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi mgombea wa chama tawala cha PNDS, Mohamed Bazoum.
Rais wa mahakama hiyo, Bouba Mahamane amesema katika taarifa kuwa, Bazoum mwenye umri wa miaka 61 na ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani amepata asilimia 55.66 ya kura zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika tarehe 21 mwezi uliopita wa Februari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mpinzani wa Bazoum, Mahamane Ousamane ambaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi 1996, amepata asilimia 44.34.
Taarifa ya Ofisi ya Rais wa Mahakama ya Katiba ya Niger imeongeza kuwa, idadi ya wapiga kura katika uchaguzi huo ilikuwa milioni 4.4 kati ya watu wote waliosajiliwa kama wapiga kura nchini humo ambao ni milioni 7.4.
Uchaguzi mkuu nchini Niger ulifanyika tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana wa 2020, ambapo mbali na wananchi kuchagua Rais, waliwachagua pia wabunge. Hata hivyo kwa kuwa hakuna mgombea urais aliyepata kura nyingi zaidi kushika wadhifa huo, ndipo awamu ya pili ikaitishwa Februari 21.
Mohamed Bazoum anatazamiwa kuapishwa kama rais wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika Aprili 4 mwaka huu kwa muhula wa miaka mitano, kuja kurithi mikoba ya Muhamadou Issofou aliyemaliza muhula wake wa pili wa miaka mitano.