Kushtadi harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika
Makundi ya kigaidi yameshadidisha harakati zao katika maeneo mbali mbali barani Afrika ambapo tukio la karibuni kabisa ni kudhibiwa na magaidi wa al-Shabab mji wa pwani wa Palma wa kaskazini mwa Msumbiji.
Awali magaidi waliishambulia Hoteli ya Amarula Palma na kuua makumi ya watu. Hoteli hiyo ipo katika mji wa Palma wa kaskazini mwa Msumbiji. Baadhi ya duru zinasema kuwa, kumefanyika mauaji makubwa dhidi ya raia katika hoteli hiyo. Wanamgambo wanaojiita al-Shabab ambao inasadikiwa kuwa wana uhusiano na kundi la kigaidi la Daesh wametangaza kuhusika na shambulio hilo.
Kwa sasa wanamgambo hao wanaudhibiti mji wa Palma huku maefu ya raia wakiripotiwa kuukimbia mji huo. Wizara ya Ulinzi ya Msumbiji imetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeanzisha operesheni kubwa ya kukomboa mji huo unaodhibitiwa na kundi hilo linalojiita al-Shabab. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Msumbiji Omar Saranga amewaambia waandishi habari huko Maputo kwamba, jeshi linapambana vikali na waasi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Palma ulioko karibu na mpaka wa nchi hiyo na nchi jirani ya Tanzania. Mji huo una akiba kubwa ya gesi inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 20.
Nchi mbali mbali za Kiafrika kwa muda sasa zimekuwa kambi za makundi ya wanamgambo na magaidi hususan makundi mawili makuu ya kigaidi yaani Boko Haram na al-Shabab. Makundi hayo yakitumia maliasili na vyanzo vya utajiri vya mataifa ya Kiafrika, yamekuwa yakiendesha harakati zake za kigaidi katika nchi mbali mbali za bara hilo kama Nigeria, Mali, Cameroon, Somalia na kadhalika, lengo likiwa ni kueneza fikra na aidilojia zao.
Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni harakati za makundi hayo ya kigaidi zinaonekana kuimarika na kuchukua mkondo mpana zaidi. Kuna sababu mbalimbali zinazotajwa na weledi wa mambo kuhusu kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika.
Sababu ya kwanza ni kushindwa kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la Asia Magharibi na akthari ya wapiganaji wake kuhamia barani Afrika. Sababu nyingine ni udhaifu wa vikosi vya ulinzi na majeshi ya mataifa ya Afrika yanayoandamwa hivi sasa na mashambulio ya kigaidi na kutokuwa na bajeti ya kutosha na suhula za kisasa za kupambana na magaidi.
Aidha kuongezeka kiwango cha umasikini na hali mbaya ya uchumi katika akthari ya nchi za Afrika ni mambo ambayo yamewafanya baadhi ya vijana kujiunga na makundi hayo ya kigaidi baada ya kuahidiwa fedha. Sababu nyingine inayotajwa na wajuzi wa mambo ni kuwa, kuweko harakati za kuwahadaa vijana kiitikadi na kuwajaza fikra za Kiwahabi na kitakfiri na baadaye kuwachukua na kwenda kuwatumia katika mashambulio ya kigaidi ambayo makundi hayo yanayataja kama vita vya jihadi. Katika upande mwingine, akthari ya viongozi wa Afrika ambao nchi zao zinakabiliwa na hujuma za kigaidi hawana azma na nia thabiti ya kupambana na makundi ya kigaidi. Hata baadhi yao wanatumia vitisho vya makundi hayo ya kigaidi kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kisiasa.
Baada ya kutokea mageuzi ya kisiasa ulimwenguni hususan katika baadhi ya nchi za Asia Magharibi ambako kunahesabiwa kuwa kitovu na makao makuu ya kundi la kigaidi la Daesh, jambo hili liliyafanya makundi ya kigaidi kama Boko Haram, Daesh na makundi mengine madogo ya kigaidi kuwa amilifu barani Afrika na kutangaza kiapo cha utiifu kwa Daesh hatua ambayo imepelekea kuimarika makundi hayo na hata kupata mafanikio zaidi katika operesheni zao za kigaidi.
Taqi al-Najar, mtafiti wa makundi ya wabeba silaha na mapigano ya silaha anasema kuhusiana na hilo: Baada ya kundi la Daesh kupoteza ngome zake kuu nchini Syria na Iraq, limelichagua bara la Afrika kama kimbilio na maficho yake kutokana na kuwa, barani humo bado kuna fursa na mazingira ya lazima ya kufanya uchochezi na kueneza fikra za kigaidi na kitakfiri.
Hali hii inashuhudiwa katika hali ambayo, kuna majeshi ya madola ya Magharibi kama Ufaransa huko barani Afrika ambayo yametumwa huko kwa kisingizio cha kwenda kupambana na ugaidi, ambapo hadi sasa hayajapata mafanikio yoyote katika vita dhidi ya ugaidi.
Ukweli wa mambo ni kuwa, hadi sasa vita dhidi ya makundi ya kigaidi vimekuwa vikitumiwa kama chombo cha kufunika ukweli wa mambo na kuimarisha uwepo wa kijeshi wa madola ya Magharibi barani Afrika, kulinda maslahi yao na hata kudumisha ushindani wa kijeshi na kiuchumi baina yao.
Bila shaka shambulio la kundi la Daesh nchini Msumbiji kwa ukubwa huu na kudhibiti mji wa Palma wa kaskazini mwa nchi hiyo ni indhari na kengele ya hatari ya uwezekano wa kushadidi harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika.
Hapana saka kuwa, kutokuweko ushirikiano wa dhati wa kijeshi na kiusalama baina ya nchi za Kiafrika na kughafilika mataifa mengine katika kutoa msaada hususan katika kipindi hiki cha kusambaa virusi vya Corona, ni jambo ambalo linaweza kuandaa mazingira mwafaka ya kukua, kupata nguvu na kujiimarisha zaidi makundi ya kigaidi na hivyo kuhatarisha zaidi usalama wa kimataifa.