May 11, 2016 07:34 UTC
  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kulihutubia Bunge la Madagascar leo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatazamiwa kulihutubia Bunge la Madagascar hii leo, kabla ya kukutana na kufanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo.

Ban Ki-moon ambaye aliwasili nchini humo jana Jumanne katika ziara rasmi ya siku mbili anatazamiwa kulihutubia Bunge hilo na kisha baadaye kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Hery Rajaonarimampianina katika Ikulu ya Iavoloha.

Miongoni mwa masuala yanayotazamiwa kupewa kipaumbele katika hotuba na mazungumzo yake na rais wa kisiwa hicho ni janga la ukame na baa la njaa. Februari mwaka huu, serikali ya Madagascar ilitangaza kuwa, watu milioni mbili katika maeneo ya vijijini wanakabiliwa na njaa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu milioni moja wanakabiliwa na njaa katika eneo la kusini mwa nchi hiyo kufuatia ukame mkali uliolikumba eneo hilo.

Kwa miaka kadhaa sasa Madagascar imekuwa ikihangaika na kufanya juhudi za kujiletea udhabiti tena tangu yalipotokea mapinduzi mwaka 2009 na kupelekea wafadhili kuikatia misaada. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2013 na kuchaguliwa Hery Rajaonarimampianina kuwa rais wa nchi hiyo, mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo ulifikia tamati. Hata hivyo mwezi Mei mwaka jana Madagascar ilikaribia kutumbikia tena katika mgogoro wa kisiasa baada ya bunge kupitisha kwa wingi wa kura pendekezo la kumuuzulu Rais Rajaonarimampianina kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni ukikwaji wa katiba na udhaifu wa kikazi.

Ban Ki-moon na ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa waliwasili Madagascar jana wakitokea Ushelisheli na Mauritius.

Tags