Madagascar yatangaza kimbunga Gezani janga la kitaifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136644-madagascar_yatangaza_kimbunga_gezani_janga_la_kitaifa
Serikali ya Madagascar jana ilitangaza kuwa kimbunga cha Gezani kilichoiathiri nchi hiyo ni janga la kitaifa. Kimbunga hicho cha kitropiki kmesasabisha vifo vya watu 43, majeruhi kadhaa, uharibifu wa miundombinu na makazi na hasara kubwa katika baadhi ya maeneo.
(last modified 2026-02-15T10:36:52+00:00 )
Feb 15, 2026 07:57 UTC
  • Kimbunga Gezani kilivyoiathiri Madagascar
    Kimbunga Gezani kilivyoiathiri Madagascar

Serikali ya Madagascar jana ilitangaza kuwa kimbunga cha Gezani kilichoiathiri nchi hiyo ni janga la kitaifa. Kimbunga hicho cha kitropiki kmesasabisha vifo vya watu 43, majeruhi kadhaa, uharibifu wa miundombinu na makazi na hasara kubwa katika baadhi ya maeneo.

Waziri Mkuu wa Madagascar, Rajaonarivelo Heritsalama, amesema akiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo kwamba kimbunga hicho kimeathiri uchumi wa nchi na maisha ya watu. Amesema serikali itajikita katika kuimarisha ustahimilivu ili kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi katika siku zijazo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Jumamosi na Idara ya Kukabiliana na Maafa na Majanga ya Kimaumbile ya Madagascar, kimbunga hicho kimesababisha vifo vya watu 43 katika wilaya 25 katika mikoa mitano ya nchi hiyo. Aidha  watu 427 wamejeruhiwa na sita hawajulikani walipo. 

Idara ya Kukabiliana na Majanga ya Kimaumbile ya Madagascar imeeleza kuwa nyumba 357,014 zimeharibiwa, watu 16,428 wamelazimika kuhama makazi yao na majengo 42,219 yamebomolewa.

Madagascar ni kati ya nchi  ambazo huathiriwa na vimbunga mara kwa mara barani Afrika na bado inasumbuliwa na athari mbaya za kimbunga cha kitropiki kwa jina la Fytia, kilichopiga wiki mbili zilizopita na kuua watu saba na kuathiri zaidi ya wengine 54,000.

Kimbunga kikali cha kitropiki cha Gezani kiliathiri maeneo ya mashariki mwa Madagascar tarehe 10 mwezi huu wa Februari, kikiwa na upepo wa kasi ya takriban kilomita 180 kwa saa na mawimbi yaliyokuwa yakizidi kasi ya kilomita 230 kwa saa. Bandari ya Toamasina iliathirika zaidi, ambapo uharibifu mkubwa wa majengo na miundombinu umeripotiwa.