Usalama waimarishwa Uganda huku Rais Museveni akitarajiwa kuapishwa kesho
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6877-usalama_waimarishwa_uganda_huku_rais_museveni_akitarajiwa_kuapishwa_kesho
Mkuu wa Polisi ya Uganda ametangaza kuwa, usalama umeimarishwa nchini humo huku Rais Yoweri Museveni akitarajiwa kuapishwa Alkhamisi ya kesho.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 11, 2016 15:37 UTC
  • Usalama waimarishwa Uganda huku Rais Museveni akitarajiwa kuapishwa kesho

Mkuu wa Polisi ya Uganda ametangaza kuwa, usalama umeimarishwa nchini humo huku Rais Yoweri Museveni akitarajiwa kuapishwa Alkhamisi ya kesho.

Inspekta Jenerali Kale Kayihura amebainisha kuwa, polisi imechukua hatua za kuimarisha usalama kwa kuwapeleka askari katika barabara kuu na njia za kuingilia mji mkuu Kampala ikiwa ni maandalizi ya kuapishwa Rais Museveni hapo kesho.

Kale Kayihura ameongeza kuwa, uimarishaji usalama huo vile vile una lengo la kukabiliana na tishio lolote tarajiwa dhidi ya usalama.

Rais Yoweri Museveni alishinda tena kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika Februari mwaka huu. Hata hivyo wapinzani nchini Uganda akiwemo hasimu wake mkuu Dakta Kizza Besigye wamekataa kutambua ushindi wa Museveni wakisisitiza kwamba, hakuchaguliwa kihalali. Hatua ya wapinzani nchini Uganda ya kukataa matokeo ya uchaguzi huo yaliambatana na maandamano hali ambayo imepelekea nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutumbukia katika mgogoro wa kisiasa.

Rais Museveni amekuwa madarakani nchini Uganda kwa zaidi ya miaka 30 sasa.

Serikali ya Uganda ikiwa na lengo la kukabiliana na maandamano ya wapinzani hivi karibuni ilipiga marufuku kanali za televisheni za nchi hiyo kuonesha moja kwa moja maandamano ya wapinzani.