Apr 08, 2021 02:34 UTC
  • Viongozi wa SADC wanakutana kujadili vita dhidi ya ugaidi Msumbiji

Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, wanakutana leo katika mazungumzo ya dharura kuhusu mzozo unaoendelea nchini Msumbiji.

Mazungumzo hayo yanafanyika katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo na yanawaleta pamoja marais wa Msumbiji, Malawi, Tanzania, Botswana, Afrika Kusini na Zimbabwe. Jumuiya ya SADC yenye nchi 16 wanachama imesema mkutano huo utajikita kwenye hatua za kukabiliana na ugaidi nchini Msumbiji. Magaidi wakufurishaji wanaofungamana na kundi la kigaidi la  ISIS walifanya uvamizi na kuuteka mji wa Palma mkoani Cabo Delgado mnamo Machi 24 ambapo makumi ya watu waliuliwa na maelfu kulazimika kuukimbia mji huo.

Mwenyekiti wa sasa wa SADC, Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi, amesema mashambulizi hayo yanatishia amani na usalama wa Msumbiji, kanda nzima na jamii ya kimataifa.

Mji wa Palma uko karibu maili sita kutoka mradi mkubwa wa gesi asili katika eneo la Afungi katika Bahari ya Hindi karibu na mpaka wa Msumbuji na Tanzania.

Jeshi la Msumbiji linasema limeukomboa kikamilifu mji huo wa Palma. Juzi Redio ya Taifa ya Msumbiji  ilitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, watu wameshaanza kurejea katika makazi yao ili kuona madhara na wizi uliofanywa na magaidi hao.

Tags