Watu wenye silaha wauwa wanajeshi 11 katika jimbo la Benue, Nigeria
Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwa wakifanya kazi jimbo la Benue katikati mwa nchi hiyo wameshambuliwa na watu wenye silaha wakiwa kazini.
Mohammed Yerima leo Ijumaa ametoa taarifa na kueleza kuwa watu waliokuwa na silaha wamewauwa wanajeshi 10 na afisa mmoja katika jimbo la Benue katikati mwa nchi hiyo.
Bado haijafahamika ni kundi gani lililohusika na shambulio hilo, hata hivyo jimbo la Benue ni sehemu ya ukanda wa kati wa Nigeria ambako makundi ya uhalifu yanatumia mashambulizi ya silaha baada ya miaka kadhaa ya machafuko ya kijamii kati ya wafugaji na wakulima.
Mwezi uliopita,Gavana wa jimbo la Benue, Samuel Ortom alieleza kuwa alinusurika kuuawa na wafugaji waliokuwa na silaha akiwa kwenye msafara. Mapigano makali kati ya wafugaji wa kabila la Fulani wanaohamahama na wakulima, wakizozania ardhi, maeneo ya kulishia mifugo na maji kwa miaka kadhaa sasa yameyaathiri maeneo ya katikati mwa Nigeria.
Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa askari usalama wa Nigeria wanakabiliana na wanamgambo wa kundi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi, magenge ya uhalifu huko kaskazini magharibi na yale yanayopigania kujitenga kusini mashariki mwa nchi hiyo.