Vijana wenye hasira washambulia wanasiasa wawili wa Kano, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6937-vijana_wenye_hasira_washambulia_wanasiasa_wawili_wa_kano_nigeria
Polisi katika jimbo la Kano nchini Nigeria imetangaza kuwa vijana wenye hasira wamewashambulia wanasiasa wawili katika jimbo hilo lililoko kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 12, 2016 10:56 UTC
  • Vijana wenye hasira washambulia wanasiasa wawili wa Kano, Nigeria

Polisi katika jimbo la Kano nchini Nigeria imetangaza kuwa vijana wenye hasira wamewashambulia wanasiasa wawili katika jimbo hilo lililoko kaskazini mwa nchi hiyo.

Msemaji wa Polisi katika jimbo la Kano, Moussa Magaji Majia amethibitisha habari ya kutokea fujo zilizofanywa na kundi la vijana wenye hasira katika mji wa Gaya ulioko umbali wa kilomita zipatazo 50 kutoka jimbo la Kano na kutangaza kuwa vijana hao wameichoma moto nyumba ya Kabiru Ibrahim Gaya na shamba la Abdullahi Mahmud, ambao ni wanasiasa wawili wa mji huo.

Magaji ameongeza kuwa hatua ya vijana hao imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kutotekeleza serikali ya Rais Muhammadu Buhari ahadi ilizotoa.

Msemaji wa polisi ya jimbo la Kano ameashiria kuwa wanasiasa hao wawili ni wanachama wa chama tawala cha Rais Buhari cha All Progressives Congress na kubainisha kwamba chama hicho kilitoa ahadi za kupunguza tatizo la kuzimwa umeme, kuongeza usambazaji wa maji na kupambana na ukosefu wa ajira katika eneo hilo.

Mbali na Rais Buhari kuahidi kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ambalo ngome yake iko kaskazini mashariki mwa Nigeria, alitoa ahadi pia ya kukabiliana na ufisadi na kuimarisha uchumi wa nchi, lakini kasi ya maendeleo imekuwa ya mwendo wa kujikongoja na hali ya uchumi wa Nigeria imezidi kuwa mbaya kutokana na kushuka bei ya mafuta, ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya pato la nchi hiyo inatokana na bidhaa hiyo.../