Shambulio la bomu laua, kujeruhi watu 20 Mogadishu, Somalia
Watu wasiopungua saba wameuawa huku wengine zaidi ya 11 wakijeruhiwa baada ya gari lililokuwa limesheheni mabomu kuripuka nje ya makao makuu ya polisi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Akithibitisha shambulio hilo, Kanali Abdiqani Mohamed Qalaf, Msemaji wa Polisi ya Somalia amesema azma ya gaidi aliyekuwa na gari hilo kuliendesha hadi ndani ya makao makuu hayo ya polisi ilitibuliwa.
Amesema iwapo asingezuiwa, watu wengi sana wangelipoteza maisha katika hujuma hiyo ya jana Jumatano. Ameongeza kuwa, wanajeshi wawili na wapita njia watatu ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo, ambalo genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limetangaza kuhusika nalo.
Dakta Hashim Suldan wa Hospitali ya Medina ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wamepokea majeruhi 13, ambapo wawili miongoni mwao wameaga dunia.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa umesema watu wapatao laki moja wamekimbia makazi yao baada ya kujiri mapigano makali katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu baina ya pande hasimu, zinazopigania suala la kurefushwa muda wa uongozi wa Rais Mohammad Abdullahi Mohammed wa nchi hiyo.
Cesar Arroyo, Kaimu Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa UN nchini Somalia amesema, watu baina ya 60,000 na 100,000 wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na ghasia hizo zilizoanza tangu Aprili 25.
Hata hivyo, Rais Farmaajo tayari amesema hataongeza muhula wake madarakani kwa muda wa miaka miwili kama alivyokuwa ametangaza hapo awali, katika kile kinachoonekana ni kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya kitaifa na kimataifa.