Somalia yahuisha uhusiano wake na Kenya baada ya kupita karibu nusu mwaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69860-somalia_yahuisha_uhusiano_wake_na_kenya_baada_ya_kupita_karibu_nusu_mwaka
Somalia imetangaza habari ya kurejesha uhusiano wake na Kenya baada ya kuukata karibu miezi sita iliyopita, ikiituhumu serikali ya Nairobi kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 07, 2021 07:45 UTC
  • Somalia yahuisha uhusiano wake na Kenya baada ya kupita karibu nusu mwaka

Somalia imetangaza habari ya kurejesha uhusiano wake na Kenya baada ya kuukata karibu miezi sita iliyopita, ikiituhumu serikali ya Nairobi kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Wizara ya Habari ya Somalia imesema katika taarifa ya jana Alkhamisi kuwa: Serikali ya Federali ya Somalia inatangaza kuwa, ili kulinda maslahi ya ujirani mwema, imerejesha uhusiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Kenya. Serikali mbili zimeafikiana kudumisha uhusiano wa kidugu baina ya pande mbili, kwa msingi wa kuheshimu uhuru na mamlaka ya kujitawala, kutoingilia masuala ya ndani ya kila upande, kudumisha usawa na kutangamana kwa amani.

Kadhalika taarifa hiyo imemshkuru Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika upatanishi wa pande mbili hizo.

Serikali ya Kenya imekaribisha hatua hiyo na kusema kuwa inatazamia kuimarisha zaidi uhusiano wake na jirani yake Somalia. Ikulu ya Nairobi imeandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amepokea 'ujumbe maalumu' kutoka kwa Amir wa Qatar uliowasilishwa na Mjumbe Maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar.

Mbali na upatanishi wa Qatar, lakini inaelekea kuwa Somalia imeafiki kuhuisha uhusiano wake na Kenya kutokana na mashinikizo ya jumuiya za kieneo hususan Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Mashariki mwa Afrika na Pembe ya Afrika IGAD.

Marais wa Kenya na Somalia katika mkutano wa nyuma

Disemba mwaka uliopita wa 2020, Somalia ilitangaza kukata rasmi uhusiano wa kidiplomasia na Kenya na kuilaumu serikali ya Nairobi kwa kujaribu kuingilia mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo. Serikali ya Somalia ilitangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya ikidai kuwa hilo ni jibu kwa kile ilichokieleza kuwa ni ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kisiasa unaofanywa na nchi hiyo na uingiliaji wake wa wazi katika masuala ya utawala ya Somalia.

Mogadishu ilitangaza kuwafukuza wanadiplomasia wote wa Kenya na kuagiza wanadiplomasia wake wote walioko Nairobi warudi nyumbani ndani ya siku saba kuanzia tarehe 15 Disemba ilipotangaza kuvunja uhusiano huo.