AU pia yasimamisha uanachama wa Mali, yatishia vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i70810-au_pia_yasimamisha_uanachama_wa_mali_yatishia_vikwazo
Umoja wa Afrika umetangaza kusimamisha uanachama wa Mali, ikiwa ni jibu kwa hatua ya wiki iliyopita ya jeshi la nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 02, 2021 02:21 UTC
  • AU pia yasimamisha uanachama wa Mali, yatishia vikwazo

Umoja wa Afrika umetangaza kusimamisha uanachama wa Mali, ikiwa ni jibu kwa hatua ya wiki iliyopita ya jeshi la nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na AU imesema kuwa, jumuiya hiyo ya kibara itawawekea watu makhsusi vikwazo iwapo utawala wa kiraia hautarejeshwa nchini humo.

Baraza la Amani na Usalama la AU limeeleza bayana kuwa, umoja huo unawataka viongozi husika wachukue hatua za haraka na za makusudi za kurejesha uongozi wa mpito wa kiraia; vinginevyo utawawekea wahusika wa mapinduzi hayo vikwazo.

Siku ya Jumapili pia, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ilitangaza kusimamisha uanachama wa Mali baada ya jeshi la nchi hiyo kufanya mapinduzi ya pili ndani ya kipindi cha miezi tisa.

Kanali Goita

Katika mapinduzi hayo ya siku chache zilizopita, maafisa wa jeshi la Mali waliwatia nguvuni Rais na Waziri Mkuu wa nchi na kuwapelekwa kwenye kambi ya jeshi nje ya mji mkuu, Bamako, hatua iliyosababisha mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.

Kanali Assimi Goita, kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali Agosti mwaka jana na kisha kuteuliwa kuwa makamu wa rais sasa amenyakua madaraka na kujitangaza kuwa rais mpya wa serikali ya mpito ya nchi hiyo, kitendo kilichobarikiwa pia na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo siku ya Ijumaa.