Kenya yairuhusu tena Somalia itumie anga yake
Kenya imetoa idhini tena anga yake itumike kwa aili ya safari za ndege kwenda na kutoka Somalia huku kukiwa na matumaini kwamba, uhusiano wa nchi hizo mbili utarejea katika hali ya kawaida.
Uamuzi huo wa wakuu wa Nairobi umechukuliwa baada ya kufungwa anga hiyo kwa mwezi mmoja huku kukiwa na matumaini kuwa, hatua hiyo itakuwa mwanzo wa kurejeshwa uhusiano wa kawaida baina ya nchi hizo mbili jirani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imesema uamuzi huo umefikiwa kwa ajili ya maslahi ya pande hizo mbili.
Hata hivyo Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya imeagiza kuwa, hatua za udhibiti wa COVID-19 zitatekelezwa kwa abiria wote kutoka Somalia kwenda Kenya, na abiria wanapaswa kuwa na uthibitisho kwamba hawajaambukizwa virusi hivyo kabla ya kuondoka au kuingia nchini.

Serikali ya Somalia imekaribisha uamuzi huo wa Kenya. Msemaji wa serikali ya Somalia Mohamed Ibrahim Moalimuu amesema kwa njia ya Twitter kuwa, hatua hiyo inaweza kurudisha katika hali ya kawaida uhusiano wa nchi hizo mbili.
Mwezi Disemba mwaka jana Somalia ilichukua uamuzi wa upande mmoja wa kukata uhusiano na Kenya ikiituhumu Nairobi kuwa inaingilia mambo yake ya ndani.