Wabeba silaha 14 waliojaribu kushambulia kituo cha polisi Nigeria wauawa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71488-wabeba_silaha_14_waliojaribu_kushambulia_kituo_cha_polisi_nigeria_wauawa
Polisi nchini Nigeria imefanikiwa kuangamiza wabeba silaha 14 waliojaribu kuvamia kituo kimoja cha polisi katika jimbo la Benue, la katikati mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2021 22:22 UTC
  • Wabeba silaha 14 waliojaribu kushambulia kituo cha polisi Nigeria wauawa

Polisi nchini Nigeria imefanikiwa kuangamiza wabeba silaha 14 waliojaribu kuvamia kituo kimoja cha polisi katika jimbo la Benue, la katikati mwa nchi.

Catherine Anene, msemaji wa polisi katika jimbo hilo amesema genge la watu 50 hivi waliokuwa wamejizatiti kwa silaha mapema jana Jumapili lilitaka kushambulia kituo cha polisi katika mji wa Katsina-Ala jimboni Benue, lakini maafisa wa polisi wakazima jaribio hilo na kuangamiza 14 miongoni mwao.

Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Anene akisema hayo na kuongeza kuwa, lengo la wabeba silaha hao lilikuwa kushambulia kituo hicho na kuwatorosha majambazi wenzao, waliokamatwa juzi Jumamosi na kuwekwa korokoroni.

Amesema baada ya kujiri makabiliano makali ya risasi, majambazi 14 walikuwa wameuawa, huku makumi ya wengine wakikimbia wakiwa na majereha.

Magenge ya wabeba silaha mbali na kuwashambulia maafisa usalama, wanawahangaisha pia wanavijiji Nigeria

Nigeria imeshuhudia wimbi la mashambulio ya makundi ya kigaidi na magenge ya wabeba silaha katika miezi ya hivi karibuni, mbali na kushtadi visa vya kutekwa nyara wanafunzi.

Wiki iliyopita, watu wasiopungua 25 waliripotiwa kuuawa katika mashambulizi mawili toafuti yanayosadikika kuwa ya kigaidi katika mkoa wa Agatu ulioko jimbo la Benue, kaskazini mwa nchi, na katika mkoa wa Bassa ulioko jimbo la Plateau, katikati mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.