Watu wenye silaha wamewateka nyara wafanyakazi wa Kichina na Kimauritania huko Mali
Watu wenye silaha wamewateka nyara raia watatu wa Kichina na wawili wa Kimauritania katika eneo la kazi la ujenzi kusini magharibi mwa Mali. Hayo yameelezwa na jeshi la Mali.
Wavamizi hao jana walishambulia eneo hilo ambko ujenzi ulikuwa ukiendelea umbali wa kilomita 55 kutoka mji wa Kwala kusini magharibi mwa Mali. Vikosi vya Ulinzi vya Mali (FAMA) vimethibitisha tukio hilo.
Mbali na kuwateka nyara wafanyakazi hao raia wa China na Mauritania, wavamizi hao waliharibu pia vifaa vya ujenzi ikiwemo winchi na kuyatelekeza malori kadhaa mali ya Kampuni ya ujenzi ya China ya COVEC n aile ya Mauritania ya ujenzi wa barabara ya ATTM.
Afisa wa jeshi la Mali amesema kuwa, raia hao wa kigeni waliotekwa nyara walikuwa wanafanyakazi ya kujenga barabara huko Kwala. Amesema kipaumbele cha jeshi la Mali ni kuona raia hao wanaachiwa huru.
Shirika la habari la Mauritania la Al- Akhbar limeripoti kuwa, watu waliokuwa na silaha waliwasili katika eneo hilo la ujenzi wakiwa kwenye pikipiki na kisha wakachoma moto vifaa vya ujenzi na matanki ya kuhifadhia mafuta kabla ya kuondoka na mateka.
Mali imekuwa ikikabiliwa na hujuma na hali ya mchafukoge inayonasibishwa na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na makundi mengine yenye mfungano na kundi la Daesh tangu mwaka 2012. Makundi hayo ya kigaidi sasa yamepanua mashambulizi na hujuma zao hadi katikati mwa Mali kutokea kwenye ngome zao katika eneo la jangwani kaskazini mwa nchi na kuendelea hadi katika nchi jirani za Burkina Faso na Niger.