Wanakijiji 100 waliokuwa wametekwa nyara Nigeria waachiliwa huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i72596-wanakijiji_100_waliokuwa_wametekwa_nyara_nigeria_waachiliwa_huru
Polisi ya Nigeria imesema, wanakijiji 100 wa eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo waliokuwa wametekwa nyara na magenge ya wabeba silaha wameachiwa huru baada ya mazungumzo iliyofanya na watekaji nyara hao waliokuwa wakiwashikilia watu hao kwa siku 42.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2021 03:22 UTC
  • Wanakijiji 100 waliokuwa wametekwa nyara Nigeria waachiliwa huru

Polisi ya Nigeria imesema, wanakijiji 100 wa eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo waliokuwa wametekwa nyara na magenge ya wabeba silaha wameachiwa huru baada ya mazungumzo iliyofanya na watekaji nyara hao waliokuwa wakiwashikilia watu hao kwa siku 42.

Magenge hayo ya watu waliojizatiti kwa silaha nzito yamekuwa yakifanya ujambazi na uharamia katika maeneo ya kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria wa kupora mali, kuiba mifugo na kuteka nyara watu ili kudai kikomboleo.

Katika mwendelezo wa vitendo hivyo, msemaji wa polisi ya jimbo la Zamfara Mohammed Shehu, ameeleza katika taarifa kwamba, mnamo tarehe 8 Julai, majambazi na maharamia hao walivamia kijiji cha Manawa, wakawateka nyara watu 100 wakiwemo wanawake na watoto na kutokomea nao kwenye maficho yao ya msituni.

Kwa kawaida, raia wanaotekwa nyara huachiwa huru kwa kikomboleo; na kwa wale ambao familia zao hushindwa kutoa kikomboleo mara nyingi huuawa; lakini kwa mujibu wa Shehu, mara hii watu hao wameachiwa huru "bila masharti yoyote" na pasi na kulipatia genge la wahalifu malipo yoyote ya fedha au mali.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ambaye analaumiwa kwa kushindwa kurejesha usalama nchini humo

Duru zilizo karibu na mazungumzo baina ya polisi na magenge hayo zimevitaarifu vyombo vya habari kuwa, majambazi na maharamia hao wamekubali kuwaachia huru wanakijiji hao 100 baada ya polisi na mamlaka za jimbo la Zamfara kuwahakikishia kuwa hawatachukuliwa hatua yoyote kwa uhalifu wa utekaji nyara huo waliofanya.

Hayo yanaripotiwa, wakati siku ya Jumatatu, askari polisi 13 waliuliwa katika jimbo hilo la Zamfara baada ya kuzingirwa na genge moja la maharamia walipokuwa wakienda kutoa ulinzi kwa raia wa kijiji kilichokuwa kikihofiwa kushambuliwa na maharamia.../