Amnesty: Jeshi la Nigeria limeua watu 115 kusini mwa nchi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, jeshi la Nigeria limeua kwa uchache watu 115 kusini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Ripoti iliyotolewa jana Alkhamisi na Amnesty International inasema kuwa, wanajeshi wa Nigeria mbali na kuua watu zaidi ya 115, lakini wamewatia nguvuni kinyume cha sheria wengine wengi na kuwakandamiza tokea mwanzoni mwaka huu hadi sasa.
Ripoti hiyo imesema askari wa Nigeria walifanya mauaji hayo kwa kisingizio cha kulipiza kisasi cha eti mauaji ya maafisa usalama yaliyofanywa na kundi linalopigania kujitenga la watu wa asili wa eneo la Biafra (IPOB), kusini mashariki mwa nchi.
Osai Ojigho, Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Nigeria amesema, "ushahidi uliokusanywa na Amnesty International umechora taswira ya kuogofya ya utumiaji nguvu kupita kiasi na maafisa usalama katika majimbo ya Imo, Anambra na Abia."
Polisi ya Nigeria imekuwa inaituhumu harakati ya Biafra kwa kuhusika na mauaji ya mamia ya watu huko kusini mashariki mwa nchi.
Ifahamike kuwa jimbo la Biafra la kusini mwa Nigeria limeshuhudia vita vibaya sana vya wenyewe kwa wenyewe kwa karibu nusu karne.