Watu 55 wapoteza maisha nchini Niger kufuatia janga la mafuriko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73450-watu_55_wapoteza_maisha_nchini_niger_kufuatia_janga_la_mafuriko
Takribani watu 55 wameaga dunia kufuatia janga la mafuriko nchini Niger huku 34 wakijeruhiwa na maelfu wakipoteza nyumba na makazi yao.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 12, 2021 23:02 UTC
  • Watu 55 wapoteza maisha nchini Niger kufuatia janga la mafuriko

Takribani watu 55 wameaga dunia kufuatia janga la mafuriko nchini Niger huku 34 wakijeruhiwa na maelfu wakipoteza nyumba na makazi yao.

Mafuriko hayo yametokea baada ya mvua kubwa kunyesha katika mji mkuu Niamey, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na roho za watu. Zaidi ya nyumba 4,000 na vibanda 200 vilianguka na mifugo 800 ilisombwa na maji, kulingana na ripoti ya Ufuatiliaji wa Huduma ya Ulinzi wa Raia.

Mikoa kadhaa nchini Niger imeathiriwa vibaya na mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea tangu mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu. Mji mkuu ni miongoni mwa miji iliyoathiriwa zaidi  na mvua ya milimita 144 iliyorekodiwa kati ya Jumanne na Jumatano.

 

Serikali ya Niger imetangaza kuwa, zoezi la uokoaji na utyoaji misaada linaendelea licha ya kuweko changamoto nyingi. Baadhi ya raia wamekwama katika baadhi ya maeneo kutokana na kutokuweko mawasiliano kutokana na barabara kutopitika katika maeneo hayo. Aidha katika baadhi ya miji madaraja yamebomolewa na mafuriko sambamba na kukatika mawasiliano ya simu na kukosekana huduma za maji na umeme.

Niger ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na janga la kimaumbile la mafuriko kila mwaka na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha. Mwaka jana 2020 na mwaka juzi pia, mamia ya watu waliaga dunia nchini humo kufuatia janga la mafuriko sambamba na kusababisha hasara kubwa hasa kwa makazi ya watu na miundombinu, huku makumi ya shule na misikiti ikisombwa na maji pia.