Wahanga wa moto wa msituni Algeria waongezeka, wafikia 90
Maafisa husika nchini Algeria wametangaza kuwqa idadi idadi ya wahanga wa moto mkubwa ulioikumba misitu nchini humo inazidi kuongezeka.
Maafisa wa serikali ya Algeria wametangaza kuwa watu 90 wakiwemo wanajeshi 33 wameaga dunia hadi sasa kufuatia moto mkubwa ulioikumba misitu ya kaskazini mwa nchi hiyo. Viongozi wa Algeria Alkhamisi iliyopita walitaja maeneo 100 nchini humo ambako moto umeanzia na kueleza kuwa moto huo ni mkubwa na kwamba wanaendelea kufanya juhudi za kuwasaka watu waliosababisha kuzuka moto.
Wananchi wa Algeria wamewakosoa viongozi wa serikali kwa kutofanya maandalizi ya mapema ya kukabiliana na maafa kama hayo.
Taarifa ya Mamlaka ya Ulinzi wa Raia ya Algeria imetangaza kuwa, akthari ya nyumba zilizokuwa zinapakana na misitu inayoteketea moto katika mkoa Tizi Ouzou ulioko yapata kilomita 150 mashariki mwa mji mkuu Algiers, zimebakia majivu kutokana na moto huo.
Kwa wiki kadhaa sasa, mioto mikubwa inaendelea kuteketeza misitu katika nchi kadhaa ikiwemo Marekani haswa katika jimbo la California, katika nchi za Ulaya hususan Ugiriki. Uturuki imepata ahueni baada ya mvua kunyesha na kuzima moto uliokuwa ukiteketeza misitu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.