Aug 20, 2021 07:28 UTC
  • Waliouawa katika shambulio la kigaidi nchini Burkina Faso waongezeka na kufika 80

Serikali ya Burkina Faso imetangaza kuwa, idadi ya watu waliouawa katika shambulio la kigaidi lililotokea nchini humo katika eneo la Sahel imefika 80.

Shambulio hilo lilitokea siku ya Jumatano likilenga msafara uliojumuisha raia, wanajeshi na askari wa utoaji misaada. Raia 59, wanajeshi 15 na askari wa utoaji misaada sita waliuawa katika hujuma hiyo.

Hayo yaliripotiwa huku duru za serikali zikitangaza kuwa, vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwaua magaidi 80 pia.

Rais Roch Marc Christian Kaboré wa Burkina Faso, siku ya Jumatano alitangaza siku tatu za maombolezo yaliyoanza jana Alkhamisi na kuamuru bendera za nchi hiyo zipepee nusu mlingoti kutokana na maafa ya roho za watu yaliyosababishwa na shambulio hilo la kigaidi.

Rais Roch Marc Christian Kaboré wa Burkina Faso

Raia wengi wa Burkina faso wameuawa katika mashambulio ya kigaidi yaliyoikumba nchi hiyo kuanzia mwaka 2015. Halikadhalika takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 230,000 wamepoteza makazi yao na kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na hujuma za makundi ya kigaidi.

Inasemekana kuwa magaidi wenye mfungamano na magenge ya DAESH (ISIS) na Al Qaeda ndio wanaohusika na hujuma hizo.../

Tags