Baada ya kuzozana na Ufaransa, Mali yaamua kununua silaha kutoka Russia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75312-baada_ya_kuzozana_na_ufaransa_mali_yaamua_kununua_silaha_kutoka_russia
Wakuu wa kijeshi nchini Mali wametangaza habari ya kuwasili nchini humo silaha kutoka Russia. Hatua hiyo imekuja baada ya kushadidi mzozo baina ya Mali na mkoloni kizee wa Ulaya, yaani Ufaransa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 02, 2021 09:53 UTC
  • Baada ya kuzozana na Ufaransa, Mali yaamua kununua silaha kutoka Russia

Wakuu wa kijeshi nchini Mali wametangaza habari ya kuwasili nchini humo silaha kutoka Russia. Hatua hiyo imekuja baada ya kushadidi mzozo baina ya Mali na mkoloni kizee wa Ulaya, yaani Ufaransa.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imetangaza kuwa, shehena ya silaha zikiwemo helikopta za kijeshi na silaha nyinginezo, zimewasili nchini Mali kutokea Russia.

Waziri wa Ulinzi wa Mali, Sadio Camara amethibitisha habari hiyo mbele ya vyombo vya habari na kusema kuwa, Bamako imenunua helikopta nne za kijeshi kutoka Russia na imepewa silaha na vifaa vingine mbalimbali vya kijeshi kama bakhshishi.

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov alisema kuwa, viongozi wa Mali wamewasiliana na mashirika binaafsi ya Russia kwa ajili ya kununua silaha za kuimarisha usalama wa nchi yao. Vile vile alisema, Ikulu ya Russia haikuhusika na mauzo hayo.

Wanajeshi wanafanya mapinduzi mara kwa mara nchini Mali

 

Tangu mwaka 2012, nchi ya Mali ya magharibi mwa Afrika imekumbwa na mapinduzi ya kijeshi na machafuko yaliyochochea kuongezeka vitendo vya kigaidi na kupata nguvu magenge yenye msimamo mikali hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

Hivi karibuni mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa ilitangaza kuondoa wanajeshi wake nchini humo. Jumamosi iliyopita, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Mali, Choguel Maiga aliishutumu Ufaransa kwa kuitelekeza nchi yake katika kipindi hiki kigumu cha kiusalama. Alitoa malalamiko hayo katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Matiafa MINUSMA pamoja na wanajeshi wa Ufaransa wamekuweko nchini Mali tangu mwaka 2013 lakini wameshindwa kuidhaminia nchi hiyo usalama wake.