Wabunge wa Kenya wataka Waziri wa Mambo ya Ndani atimuliwe
Baadhi ya Wabunge wa Kenya wanajianda kumuondoa mamlakani Waziri wa Masuala ya Ndani wa nchi hiyo, Fred Matiang'i.
Wabunge hao wakiongozwa na mbunge wa Nyali, Mohamed Ali, wanamtuhumu Matiang'i kuwa ametumia vibaya mamlaka yake ikiwa ni pamoja na kukiuka Sura ya Sita ya Katiba. Ripoti zinaonesha kuwa wabunge 92 tayari wametia saini na kuunga mkono muswada huo
Wengi kati ya wabunge waliotia saini muswada huo wa kumtimua Waziri wa Masuala ya ndani, Fred Matiang'i, wanamuunga mkono Naibu Rais Kenya, William Ruto.
Muswada huo ulidhaminiwa na mbunge wa Nyali, Mohamed Ali, ambaye anatarajiwa kuwasilisha notisi katika majengo ya Bunge. Waziri huyo mwenye ushawishi mkubwa katika serika ya Kenya anatuhumiwa kuwa amekiuka vipengee vya Katiba vinavyohusu uongozi na uadilifu.
Misingi mingine iliyotolewa ya kumtimua waziri huyo ni pamoja na kusababisha ufa kati ya mamlaka ya Bunge na ile ya Ofisi ya Rais.
Ilani hiyo sasa itasuburi kuidhinishwa na Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Justin Muturi.