AU yaunga mkono kuundwa kikosi cha pamoja nchini Somalia
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetangaza kuunga mkono pendekezo la kuundwa kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa nchini Somalia, kitakachochukua nafasi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (Amisom), iwapo wazo hilo litapasishwa.
Muda wa kuhudumu wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia unamalizika mwanzoni mwa mwaka ujao 2022, ambapo wanajeshi 22,000 wa kikosi hicho wanatazamiwa kuondoka katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Mwezi Juni mwaka huu, AU ilirefusha muda wa kuhudumu askari hao wa kieneo nchini Somalia kwa muda wa miezi sita, yaani hadi Januari mwakani.
Azimio hilo la Baraza la Amani na Usalama la AU la kuunga mkono mpango wa kuundwa kikosi cha pamoja na Umoja wa Mataifa nchini Somalia sharti lipasishwe na Baraza la Usalama la UN.
Likipasishwa, operesheni za kiusalama nchini Somalia zitakuwa zinafuatiliwa na kusimamiwa na Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka ujao 2022. Serikali ya Federali ya Somalia imeonekana kutounga mkono pendekezo hilo, ikisisitiza kuwa mpango huo hautasaidia chochote katika kuimarisha usalama wa nchi hiyo.
Kwa sasa wanajeshi 22,000 wa Amisom walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa Amisom ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.