Faki Mahamat: Utegemezi unatishia uhuru wa kujitawala AU
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema mataifa ya bara hilo yanapaswa kushirikiana na kufanya kazi pamoja, ili kuhakikisha kuwa yanaondokana na utegemezi na vilevile yanajikomboa kifedha.
Moussa Faki Mahamat alisema hayo jana Alkhamisi katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa 39 wa Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, yalipo makao makuu ya AU.
Amesema hatua ya umoja huo kutegemea ufadhili na fedha za misaada, inatishia uhuru wa taasisi hiyo kujitawala, kujiendeshea mambo yake namna inavyotaka na kujianishia mustakabali wake.
Mahamat ameeleza bayana kuwa, daima bajeti ya AU huwa imebanwa na huwa hawana budi kupunguza matumizi na kutoa kipaumbele kwa masuala yenye umuhimu zaidi, jambo ambalo linawalazimisha kutegemea misaada na ufadhili.
Hii ni mara ya kwanza ndani ya miaka miwili kwa mkutano wa Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika kufanyika kwa washiriki kuhudhuria ana kwa ana. Mikutano kadhaa imefanyika kwa njia ya intaneti kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19.
Uamuzi wa upande mmoja uliochukuliwa na mkuu huyo wa Kamisheni ya AU wa kuupatia utawala wa Kizayuni wa Israel hadhi ya kuwa mwanachama mtazamaji katika taasisi hiyo kuu ya bara la Afrika, ni miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano huo.