Watumishi wa umma ambao hawajachanja Zimbabwe kutoruhusiwa kazini
(last modified Sat, 16 Oct 2021 02:32:01 GMT )
Oct 16, 2021 02:32 UTC
  • Watumishi wa umma ambao hawajachanja Zimbabwe kutoruhusiwa kazini

Kuanzia Jumatatu ijayo, wafanyakazi wa serikali na watumishi wote wa umma ambao hawajapiga chanjo ya kukijikinga na ugonjwa wa COVID-19 hawataruhusiwa kuingia kazini nchini Zimbabwe.

Waraka uliosainiwa na Jasper Chimedza, Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Afya nchini Zimbabwe umesisitiza kuwa, wafanyakazi wote wa serikali ambao hawatawasilisha vyeti vya kuthibitisha kuwa wamepiga chanjo ya Corona, hawajaturuhusiwa katika sehemu zao za kazi kuanzia Jumatatu.

Waraka huo ambao umesambazwa katika ofisi na idara za serikali nchini humo umebainisha kuwa, watumishi wa umma ambao watafeli kufika kazini kwa kukiuka agizo hilo la kuwataka wachanje watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Septemba mwaka huu, Ziyambi Ziyambi, Waziri wa Sheria wa Zimbabwe aliwaasa wafanyakazi wote wa idara za serikali na ofisi za umma nchini humo kupata chanjo dhidi ya COVID-19 ndani ya mwezi mmoja; na kwa wale wasiotaka kufanya hivyo wanapaswa kujiuzulu.

Mhudumu wa afya akimshughulikia mgonjwa wa Corona

Alisisitiza kuwa, hatua hiyo inalenga kukabaliana na msambao wa virusi vya Corona na wakati huo huo kukabiliana na changamoto ya baadhi ya watu wanaosita kupata chanjo hiyo ambayo kwa sasa ndilo chaguo bora la kukabiliana na maradhi hayo.

Kufikia sasa, nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imenakili kesi zaidi 132,000 za ugonjwa huo hatari wa kuambukiza, na vifo zaidi ya 4,600 vya maradhi hayo yanayoendelea kuihangaisha dunia kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa.