Kutangazwa hali ya hatari nchini Ethiopia
Mvutano kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) umepamba moto katika miezi ya karibuni; hatua iliyoipelekea serikali ya Addis Ababa kutangaza hali ya hatari nchini humo kufuatia kusonga mbele kupya waasi wa Tigray.
Harakati ya Ukombozi ya watu wa Tigray imetangaza kuwa wapiganaji wake wanaidhibiti miji miwili muhimu ya Dessie na Kombolcha. Kutekwa na waasi wa harakati ya TPLF mji wa Kambolcha kunahesabiwa kuwa mafanikio ya kimkakati. Mji huo mkubwa unapatikana katika barabara kuu katika umbali wa takribani kilomita 380 kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa; na uko katika nukta ya kusini upande wa mji wa Amhara ambako wapiganaji wa TPLF walifikia tangu walipoingia huko mwezi Julai mwaka huu. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vitakabiliana kwa nguvu na uwezo wake wote na wapiganaji wa TPLF na kueleza kuwa: Kuna changomoto nyingi mbele yetu lakini ninatamka wazi kuwa tutaibuka na ushindi mkubwa."
Kwa muda sasa eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia limekumbwa na mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF). Jamii ya walio wachache ya wakazi wa Tigray inaunda asilimia 6 ya jamii nzima ya Ethiopia. Jamii hiyo inaamini kuwa serikali kuu ya Ethiopia haizingatii maslahi yao. Ni kwa sababu hiyo ndio maana hatua za kupigania kujitenga wakazi wa eneo la Tigray zimeongezeka. Mapigano kati ya vikosi vya serikali na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) yalianza tangu Novemba Nne mwaka jana 2020 na kushtadi huku viongozi wa Tigray wakiendesha uchaguzi wa mabaraza ya miji na serikali za mitaa kinyume na matakwa ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. Abiy Ahmed anaona kuwa serikali ya Tigray inaenda kinyume cha sheria na kuwa inafanya kila iwezalo kulidhibiti eneo hilo kwa nguvu. Hali hiyo imeipelekea serikali ya Addis Ababa kuingia vitani na harakati ya TPLF. Abiy Ahmed aliwahi kusema kuwa oparesheni hiyo itakuwa ya muda mfupi lakini mapigano yangali yanaendea hadi sasa na hasa yameshtadi katika miezi ya karibuni.
Ethiopia ni nchi ya pili yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika ikiwa na watuu zaidi ya milioni 100; mbapo nchi hiyo imekuwa ikitazamwa kama kigezo cha kurejea demokrasia kabla ya kuongezeka hivi karibuni hali ya mivutano nchini. Wakati huo huo kuongezeka mivutano na mapigano kati ya serikali kuu na wakazi wa eneo la Tigray na kupelekea kuuawa wakazi wa eneo hilo kumemfanya Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019 kupoteza sifa yake njema kama mlinda amani.
Katika upande mwingine, mivutano ya kisiasa inaendelea huko Ethiopia katika hali ambayo uingiliaji wa nchi ajinabi katika nchi hiyo muhimu ya Kiafrika unaongezeka pia. Kuwepo mashirika ya kigeni ya Kizayuni katika mradi wa ujenzi wa bwawa la Reinassance na pia misimamo inayochukuliwa na Marekani kuhusu mgogoro wa Tigray kumeweka wazi pakubwa jitihada na njama za nchi za Magharibi za kutaka kujipenyeza na kuingilia masuala ya nchi hiyo; ambapo tayari Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza kufuta mapatano ya kibiashara na Ethiopia na hivyo kuandaa uwanja wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.
Mapigano yanayojiri kaskazini mwa Ethiopia hadi sasa yamesababisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbzi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na njaa. Jitihada za usuluhishi za taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Tigray zimepingwa na pande zinazozozana. Hii ni katika hali ambayo hali ya mambo katika eneo hilo ni mbaya kiasi kwamba Martin Griffiths Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu ameutaja mgogoro wa eneo la Tigray kuwa ni fedheha kwa dhamira ya kimataifa."
Inaonekana kuwa aghalabu ya wakazi wa Tigray na wa maeneo jirani yake watauawa au kulazimika kuwa wakimbizi iwapo hali ya mambo itaendelea na kutashuhudiwa pia ongezeko la watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu. Wakati huo huo kutangazwa hali ya hatari huko Ethiopia kunaweza kuwa kengele ya tahadhari kwa ajili ya kushtadi mapigano nchini humo na si kutekelezwa juhudi za kuutatua mgogoro katika eneo la Tigray.