Mjumbe wa AU aonya kuhusu kuzidi kuwa mbaya mgogoro wa Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i76710-mjumbe_wa_au_aonya_kuhusu_kuzidi_kuwa_mbaya_mgogoro_wa_ethiopia
Mjumbe wa Umoja wa Afrika katika masuala ya Pembe ya Afrika ametadharisha kuwa, mlango wa fursa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Ethiopia unazidi kufungika siku baada ya siku.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 09, 2021 04:46 UTC
  • Mjumbe wa AU aonya kuhusu kuzidi kuwa mbaya mgogoro wa Ethiopia

Mjumbe wa Umoja wa Afrika katika masuala ya Pembe ya Afrika ametadharisha kuwa, mlango wa fursa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Ethiopia unazidi kufungika siku baada ya siku.

Olusegun Obasanjo alitoa indhari hiyo jana Jumatatu katika ujumbe wake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya kufanya mazungumzo na Rais na Waziri Mkuu wa Ethiopia, pamoja na viongozi wa makundi ya waasi wa eneo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Obasanjo ambaye amewahi kuwa rais wa Nigeria amesema, pande husika katika mgogoro wa Tigray katika nyakati tofauti zimekiri kuwa, mzozo uliopo ni wa kisiasa na unahitaji suluhu ya kisiasa kupitia njia ya mazungumzo.

Amesema atatembelea maeneo ya Amhara na Afar yanayopakana na Tigray, ili kuyawianisha maoni ya viongozi wa maeneo hayo kuhusu "kuondoka kwa askari katika maeneo yasio yao, na jinsi ya kufikisha misaada ya kibinadamu katika maneo husika."

Mapigano Tigray

Hii ni katika hali ambayo, wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) ya jimbo la Tigray wanaoendesha mapambano dhidi ya serikali kuu ya Ethiopia wameapa kuendeleza jitihada zao za kusonga mbele na kuingia mji mkuu, Addis Ababa.

Mapigano yanayoendelea huko Tigray mbali na kuua maelu ya watu hadi sasa, lakini pia yamesababisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na ukosefu wa chakula.