Kiongozi wa wanaotaka kujitenga Biafra (IPOB), kufikishwa mahakamani leo
(last modified Wed, 10 Nov 2021 06:32:42 GMT )
Nov 10, 2021 06:32 UTC
  • Kiongozi wa wanaotaka kujitenga Biafra (IPOB), kufikishwa mahakamani leo

Kiongozi wa Watu wa Asili wa Biafra (IPOB), wanaotaka kujitenga eneo la kusini mashariki mwa Nigeria, anatazamiwa kurejeshwa mahakamani hii leo Jumatano katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.

Nnamdi Kanu anayengoza chama cha Indigenous People of Biafra (IPOB), anakabiliwa na tuhuma za "ugaidi", uhaini na kueneza uongo dhidi ya Rais Muhammadu Buhari, hasa kupitia matangazo kwenye kituo cha Radio Biafra na mitandao ya kijamii. 

Baada ya kukaa kizuizini kwa miaka miwili, Kanu alitoweka Aprili 2017 baada ya kuachiwa huru kwa  dhamana. Wafuasi wake waliilaumu serikali ya Nigeria lakini yapata mwaka mmoja baadaye alijitokeza kwa njia ya kustaajabisha akiwa Israel.

Nnamdi Kanu akiwa Israel

Mwezi Juni mwaka huu, Nnamdi Kanu ambaye pia ana uraia wa Uingereza, alikamatwa nchini Kenya na kurejeshwa Nigeria. Tangu wakati huo, chama cha IPOB kimekuwa kikifanya mgomo wa  kuketi nyumbani kila siku ya Jumatatu na wakati mwingine katika siku zingine za wiki ili kueleza upinzani wake dhidi ya kuendelea kufungwa kiongozi wa chama hicho.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 30 ambavyo vilichochewa na matakwa ya kujitenga eneo la Biafra vilimalizika mwaka 1970. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni moja waliaga dunia katika vita hivyo. Eneo hilo ambalo ni makazi ya watu wa jamii ya Igbo, kabila la tatu kwa ukubwa nchini Nigeria, liliunganishwa tena na nchi hiyo lakini harakati za kutaka kujitenga zilianza tena baada ya mabadiliko ya utawala mwezi Mei 1999.

Wanachama wa IPOB wanasema eneo hilo limetengwa kiuchumi na kisiasa tangu baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe.