Jeshi la Sudan Kusini: Tumeukomboa mji muhimu kutoka mikononi mwa Jeshi Jeupe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125492-jeshi_la_sudan_kusini_tumeukomboa_mji_muhimu_kutoka_mikononi_mwa_jeshi_jeupe
Jeshi la Sudan Kusini limetangaza kuwa limeukomboa mji muhimu katika jimbo la Upper Nile ambao ulikuwa umetekwa na wanamgambo wa kabila la Nuer mwezi Machi katika mapigano ambayo yalipelekea kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar na kuibua mzozo mkubwa wa kisiasa nchini humo.
(last modified 2025-04-22T10:50:38+00:00 )
Apr 22, 2025 08:46 UTC
  • Jeshi la Sudan Kusini: Tumeukomboa mji muhimu kutoka mikononi mwa Jeshi Jeupe

Jeshi la Sudan Kusini limetangaza kuwa limeukomboa mji muhimu katika jimbo la Upper Nile ambao ulikuwa umetekwa na wanamgambo wa kabila la Nuer mwezi Machi katika mapigano ambayo yalipelekea kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar na kuibua mzozo mkubwa wa kisiasa nchini humo.

Hata hivyo, wasemaji wa jeshi la serikali na wa kundi linalojiita Jeshi Jeupe (White Army), ambalo chama cha Machar kinakanusha kuliunga mkono, wamesema mji huo wa Nasir ulikombolewa siku ya Jumapili bila kutokea mapigano yoyote.

"Tulikuwa tukichukua uamuzi wa kujiondoa," amesema Honson Chuol James, msemaji wa kundi la Jeshi Jeupe na akaongeza kuwa watu 17 waliuawa wakati wa mashambulizi makubwa ya mabomu katika kijiji cha karibu cha Thuluc.

Msemaji wa jeshi la serikali Lul Ruai Koang yeye amesema, wanajeshi waliweza kuepuka shambulizi la kuvizia la Jeshi Jeupe huko Thuluc kutokana na kufunga usaidizi wa anga.

Kuzuiliwa Machar chini ya kifungo cha nyumbani, kwa tuhuma za kujaribu kuzusha uasi kwa kuwaunga mkono wa wanamgambo wa Jeshi Jeupe huko Upper Nile, kumezusha hofu kimataifa ya kuzuka upya migogoro nchini Sudan Kusini kwa misingi ya kikabila.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mapema mwezi huu chama cha Machar cha SPLM-IO kilionekana kuanza kusambaratika baada ya kundi moja kutangaza kuwa limemuondoa Machar kama mwenyekiti wa chama kwa muda, huku mrengo mwingine wa chama hicho ukisisitiza kuwa unaendelea kuwa mtiifu kwa kiongozi wao huyo aliyeko kizuizini.../