Kifo cha FW De Klerk chaibua hisia tofauti nchini Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i76818-kifo_cha_fw_de_klerk_chaibua_hisia_tofauti_nchini_afrika_kusini
Kifo cha rais wa mwisho mweupe wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Frederik Willem (FW) de Klerk kimeibua hisia tofauti baina ya raia na wanasiasa ndani na nje ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 12, 2021 04:23 UTC
  • Kifo cha FW De Klerk chaibua hisia tofauti nchini Afrika Kusini

Kifo cha rais wa mwisho mweupe wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Frederik Willem (FW) de Klerk kimeibua hisia tofauti baina ya raia na wanasiasa ndani na nje ya nchi hiyo.

De Klerk ambaye alishiriki katika mjadala wa kukomeshwa utawala wa wazungu wachache na kukabidhi madaraka kwa amani kwa serikali ya wazalendo weusi, alifariki dunia Alkhamisi na jana akiwa na umri wa miaka 85, baada ya kuugua saratani.

Frederik Willem de Klerk alipata sifa duniani kwa hatua yake ya kufuta ubaguzi wa rangi na alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel akishirikiana na shujaa wa uhuru wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela mwaka wa 1993. Mwaka uliofuata Mandela alishinda uchaguzi wa kwanza wa Afrika Kusini ulioshirikisha watu wa rangi zote akiongoza chama cha African National Congress (ANC).

Mzee Mandela na De Klerk wakipokea Tuzo ya Nobel

Hata hivyo nafasi na mchango wa de Klerk katika kipindi cha mpito kuelekea kwenye demokrasia bado inazusha mjadala mkubwa karibu miaka 30 sasa baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Raia wengi weusi wa nchi hiyo walikasirishwa na kushindwa kwake kuzuia ghasia za kisiasa katika miaka ya msukosuko ya kuelekea uchaguzi wa 1994 ulioshirikisha watu wa rangi zote, huku wazungu wa mrengo wa kulia, ambao walitawala nchi kwa muda mrefu chini ya Chama cha Kitaifa cha de Klerk, wakimuona kuwa ni msaliti wa fikra yao ya kuwa bora watu weupe kuliko mbari nyingine. 

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema: "De Klerk alikuwa na 'mchango' muhimu katika kuleta demokrasia nchini", na ametoa salamu za rambirambi kwa familia ya rais huyo wa zamani. 

Taasisi ya Nelson Mandela imetoa tarifa ikisema: De Klerk amebakisha 'urithi mkubwa', jambo ambalo Waafrika Kusini wanatakiwa kulishughulikia kwa wakati huu.”

Kwa upande wake kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) ambacho ni cha tatu kwa ukubwa nchini Afrika Kusini, Julius Malema, amesema De Klerk hatakiwi kutajwa kama "rais wa zamani" bali kama "rais wa zamani wa utawala wa ubaguzi wa rangi".